Kanisa halina budi kushikamana na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa
kuliongoza Kanisa Katoliki, amebahatika kufanya mahojiano maalum na Kituo cha Radio
cha Bajo Flores, FM 88.1 kinachorusha matangazo yake nchini Argentina. Haya ni mahojiano
yaliyofanywa kwa njia ya Video, ambamo Baba Mtakatifu anakazia uwepo wa Kanisa miongoni
mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ili waweze kuonja huruma na
upendo wa Mungu.
Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa waamini kujitokeza kifua
mbele kutangaza Injili ya Furaha hadi miisho ya dunia. Anawakumbuka kwa namna ya pekee,
Mapadre, Watawa na Waamini walei wanaoendelea kushuhudia uwepo wa Kanisa kati ya Maskini
kwa njia ya huduma makini huko Argentina. Huu ni utume ambao anaufahamu kwa kina kwani
ulikuwa ni sehemu ya mikakati yake ya kichungaji alipokuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu
la Buenos Aires.
Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa huduma ya elimu makini
kwa maskini, kama nyenzo msingi inayoweza kuwaletea ukombozi wa kweli dhidi ya ujinga
na umaskini, tayari kupambana na mazingira katika maisha yao. Uwepo wa Mapadre na
Watawa usaidie mchakato wa kuwasindikiza vijana katika makuzi na malezi makini kwani
huu ni utume unaopewa kipaumbele na Mama Kanisa. Hawa ni viongozi wa Kanisa wanaotaka
kujenga mshikamano wa upendo na maskini kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki
zao msingi.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema
kuguswa na mahangaiko ya jirani zao, tayari kushikamana kwa upendo katika huduma,
kwani binadamu wanategemeana na kukamilishana, hakuna mtu anayeweza kujigamba kwamba,
anajitosheleza kwa yote. Vyombo vya habari vijitahidi kutangaza na kueneza ukweli,
kwa kutoa kipaumbele kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kwani
hata wao wanapaswa kusikika.
Baba Mtakatifu anasema kati ya mambo yanayompatia
ugumu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kukaa ofisini
na kuanza kushughulikia makaratasi, ni jambo ambalo anasema limeendelea kumtesa katika
maisha yake kama Askofu na sasa kama Papa. Anawaalika waamini pamoja na watu wote
wenye mapenzi mema kusali kwa ajili yake. Kwa kweli, watu kutoka sehemu mbali mbali
za dunia wanaendelea kusali na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na
utume wake.