2014-03-14 07:49:31

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima, Mwaka A wa Kanisa


Tunaendelea na kipindi cha Kwaresima, tafakari masomo Dominika II mwaka A. Neno la Mungu latualika kutafakari juu ya wito wetu kielelezo kikiwa wito wa Abramu. RealAudioMP3

Mpendwa msikilizaji, Somo la kwanza latuonesha jinsi historia ya wokovu ilivyosimika miguu, pale Mungu anapomwita kwanza Abramu awe Baba wa imani. Kwa kumwita Abramu Mungu atuonesha lile pendo na namna yake ilelile ya kumwendea mwanadamu kabla ya mwanadamu hajanyanyua mguu kumtafuta Mungu. Tunatambua kuwa Abramu aliishi Mesopotamia miaka 2000KK na katika nchi yake hiyo kulikuwa na kila aina ya utajiri, hata hivyo kulikuwa na machafuko wakati fulani.

Mungu anamwita, na Abramu anasikia sauti ya Mungu pamoja na kwamba kulikuwa na kelele nyingi katika nchi yake hiyo. Abramu anasikia sauti ya Mungu kwa sababu ya imani yake na anaondoka kadiri ya matakwa ya Mungu. Hata hivyo yafaa kujiuliza hivi ilikuwa rahisi kuondoka hapo nyumbani na kuelekea nchi asiyoijua? Kwa vyovyote vile alipata ugumu fulani lakini kwa sababu ya imani aliondoka!

Mpendwa msikilizaji, Abramu anaitwa kuacha uhakika wa maisha na kwenda ambapo hakuna uhakika, hili ni jambo la ajabu, lakini linasukumwa na ahadi za Mungu yaani atapewa ardhi mpya, atakuwa na ustawi na baraka tele. Katika hili twajifunza nini! Twajifunza maisha ya kujitoa kiaminifu na kujibandua katika fikira zetu za kizamani, yaani, pingamizi kwa imani na kuanza maisha mapya, maisha yenye baraka toka kwa Mungu. Safari ya Abramu ni safari yetu ya imani, ndiyo kwaresima yetu yaani kubadilika na kubadilisha maisha yetu. Yote haya yatawezekana katika tumaini na imani kama Abramu alivyotumaini bila kuona.

Katika somo II Mt. Paulo anamtia moyo Mt. Timoteo, Askofu wa Efeso, kuvumilia mateso na taabu, pamoja na changamoto za kitume katika jumuiya yake. Wakati Mt. Paulo anaandika ujumbe huu, kulikuwa na migongano na malumbano katika Efeso na hivi kuleta hatari kwa maisha ya kitume. Basi Mt. Paulo akisimika ujumbe wake katika Bwana wetu Yesu Kristu, anasema, mauti yatabatilishwa katika yeye, kumbe Mt. Timoteo asiwe na mashaka, cha msingi amtegee yeye aliyemwita katika mwito mtakatifu.

Katika somo la Injili mwinjili Matayo atuambia Yesu ni nani akitumia alama na ishara kadhaa katika Injili yake. Leo Bwana yuko mlimani, akiwa na Mitume watatu na anageuka sura, mavazi yanakuwa meupe na hatimaye kunaonekana Bwana akizungumza na Musa na Eliya. Si hayo tu bali kutatokea wingu jeupe na sauti kutoka katika wingu hilo ikitangaza huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu ninayependezwa naye, msikieni yeye.

Katika ishara ya mlima tunatambua mara zote Bwana anapotaka kutenda jambo muhimu katika Injili ya Mathayo daima anakwenda mlimani. Ndiyo kusema, matukio ya mlimani tuyafamuyo ni kama ifuatavyo: Tangazo la heri Nane, majaribu tuliyoyasikia katika Dominika iliyopita, ongezeko la Mikate, na mwisho wa Injili Bwana mfufuka anapowatuma Mitume kwenda duniani kote anakutana nao mlimani. Jambo hili tunalikuta katika Agano la Kale ambapo Musa atathibitishiwa Agano na kupokea amri za Mungu akiwa mlimani, (Kut. 24:12).

Mpendwa mwana wa Mungu, kuhusu habari ya kuwa na Mitume pale mlimani si jambo jipya bali lina uhusiano na uwapo wa Musa mlimani pamoja na Yoshua wakati wengine wakiachwa chini ya mlima. Pale mlimani Musa atafunikwa na wingu na utukufu wa Mungu utatua mlimani Sinai kwa SIKU SITA na siku ya saba, Mungu anamwita Musa toka wingu lile. Mpendwa msikilizaji matukio haya yanajionesha katika Bwana, kumbe Mwinjili Matayo ataka kutumbia Kristu Masiha, ni Musa mpya, ni yule atakayeongoza taifa jipya la Mungu linalowakilishwa na Mitume watatu pale mlimani. Ni yule anayetoa sheria mpya na ukamilifu wa ufunuo wa Mwenyezi Mungu.

Mpendwa msikilizaji Bwana anaonekana katika mavazi meupe, ikiwa ni alama ya uwapo wa Mungu katika nafsi ya Yesu Kristu, hili linaambatana na wingu jeupe ambao lamwakilisha Mungu. Kumbukeni Waisraeli wanapotoka utumwani Misri wataongozwa na wingu jeupe, ambayo ni alama na ishara wazi ya ulinzi wa Mungu katika safari yao hiyo ya kurudi nyumbani, (Kut. 13:20-22).

Mpendwa msikilizaji, Mwinjili anaweka pia mbele yetu ishara ya sauti toka juu, ambayo tuliisikia wakati wa ubatizo wa Bwana, lakini katika tukio hili ataongeza MSIKIENI YEYE. Ni Mungu anayesema na watu wake kwa njia ya Mwanae mpenzi. Basi unaalikwa katika kwaresima hii kusikia anachosema Bwana kwa njia ya Neno lake. Ishara nyingine muhimu ni uwepo wa Musa na Elia.

Hawa wanawakilisha Agano la Kale na hivi wanapotoweka wanaonekana Mtume watatu wakimtazama Bwana. Ndiyo kusema Kristo Masiha ndiye sasa sheria mpya kwa ajili ya Agano Jipya, sheria tutakiwayo kuitazama na kuishika na hivi msikieni yeye. Wakati ndo huu, wakati wa kupanda, wakati wa kupalilia na kuondoa magugu na vinyemelezi katika mashamba ndiyo mioyo yetu.

Mpendwa msikilizaji, jambo jingine la kutusaidia kukua kiroho ni lile la Mtakatifu Petro kumwambia Bwana, yakuwa, yafaa kukaa hapo mlimani na kujenga vibanda vitatu. Katika hili Petro anadhani Yesu ni mtu mkubwa katika uzito uleule wa manabii, wakati kwa hakika ni mkuu kuliko wao, ni Mwana wa Mungu na hivi kila mmoja analikwa kumsikia yeye tu.
Mpendwa mwana wa Mungu, kwako wewe wajibu ni kutafakari haya yote na kuyaweka moyoni lakini hasa kujenga usikivu wa kudumu, hujachelewa katika kwaresima hii mpaka mwisho wa maisha yako hapa duniani.

Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.