2014-03-14 11:26:58

Kanisa ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!


Kanisa linapaswa kuonesha huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kuwavuta watu zaidi ili waweze kujenga imani na matumaini ya kukutana na Mungu kwa njia ya Kanisa linaonesha moyo wa ukarimu na mapendo. Waamini wajenge na kuimarisha urafiki wao na Yesu Kristo, kama alivyofanya yule mwanamke mdhambi kwa kumpaka marhamu ya nardo safi ya thamani, jambo lililowafanya baadhi ya watu kuchukizwa na kitendo hiki!

Hapa Yesu alikuwa nyumbani kwa Simeoni mkoma na kadiri ya Wayahudi hapa palikuwa ni najisi, lakini Yesu alionesha moyo wa upendo na ukarimu hata kwa wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kuwaonjesha upendo na huruma ya Baba yake wa mbinguni! Tukio hili linafanyika mjini Bethania, kielelezo cha ukarimu na huruma ya Mungu.

Yote haya ni matukio yaliyokuwa yanamwandaa Yesu kukabiliana na Fumbo la Msalaba, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Katika mazingira kama haya, yule mwanamke mdhambi anamwonjesha Yesu upendo usiokuwa na mawaa na anauandaa mwili wake kwa ajili ya maziko. Mwanamke huyu alitoa sadaka kubwa kwa ajili ya upendo kwa Yesu, kwani watu wengine walivutwa zaidi na mantiki ya soko na masuala ya kiuchumi, lakini Yesu anamsifia sana yule mwanamke kwa ushupavu na upendo aliomwonesha, ukawa ni cheche za toba na wongofu wa ndani.

Hivi ndivyo alivyokazia Monsinyo Angelo De Donatis wakati akitoa mafungo kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasaidizi wake wa karibu; mafungo ambayo yamehitimishwa rasmi Ijumaa, tarehe 14 Machi 2014. Anasema, Bikira Maria ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu, aliyethubutu kujiaminisha mikononi mwa Mungu na hatimaye, akawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno la Mungu aliyefanyika mwili.

Changamoto kwa kila mwamini ni kuhakikisha kwamba, anagundua ujasiri wa imani ili kuondokana na woga usiokuwa na tija wala mashiko katika maisha ya mwamini.







All the contents on this site are copyrighted ©.