Jifungeni kibwebwe kulitegemeza Kanisa Barani Afrika!
Kanisa Barani Afrika halina budi kuhakikisha kwamba, linajifunga kibwebwe katika sera
na mikakati yake ya kichungaji inayopania kulitegemeza Kanisa badala ya kuendelea
kubweteka kwa kutegemea misaada kutoka ng'ambo jambo ambalo kwa sasa limepitwa na
wakati. Haya ni kati ya mambo yaliyoibuliwa wakati wa Kongamano lililoandaliwa na
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, kwa ajili
ya Makatibu wakuu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kikanda na Kitaifa huko Johanesburg,
Afrika ya Kusini.
Hii ni changamoto iliyotolewa na Padre Nicholas Afriyie,
Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana wakati wa kuchangia katika mada kwenye
Kongamano hilo. Umefika wakati kwa SECAM kuanzisha kitengo ambacho kitatafuta fedha
kutoka Barani Afrika kwa ajili ya utekelezaji wa mikakati ya maendeleo na ustawi wa
Familia ya Mungu Barani Afrika.
Kitengo hiki kinapaswa kutambua na kuonesha
mahali ambapo Kanisa linaweza kupara rasilimali ya kugharimia miradi yake na uwezekano
uliopo ndani ya Kanisa Barani Afrika. Waamini wakijizatiti inawezekana kabisa kulitegemeza
Kanisa Barani Afrika, hasa kwa kuwahusisha waamini walei, kwa kuwa na nidhamu, ukweli
na uwazi katika matumizi ya mali ya Kanisa.
Katika kongamano hili wajumbe pia
wamefundishwa umuhimu na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuwatangazia
watu Habari Njema ya Wokovu. Wajumbe wameweka mikakati na ratiba ya Maadhimisho ya
Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika, hapo mwakani baada ya kuthibitishwa na SECAM. Kongamano
hili limewashirikisha viongozi wa Kanisa kutoka Afrika ya Kusini na wadau wengine
wa SECAM katika utekelezaji wa miradi na mikakati ya SECAM Barani Afrika.