Yaliyojiri katika maisha na utume wa Papa Francisko
Kardinali Jorge Bergoglio aliyechagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi, fukara,
mpenda amani na mtunza mazingira ni Papa wa 265 aliyeuanza utume wake kama Khalifa
wa Mtakatifu Petro kwa moyo wa unyenyekevu na unyofu wa kiinjili. Ni Papa wa kwanza
kuchaguliwa kutoka katika Shirika la Wayesuit na Papa wa kwanza kutoka Kanisa la Amerika
ya Kusini.
Papa Francisko
katika mahubiri yake ya mwanzo kabisa, ameonesha mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji
kwa Kanisa ambalo linapaswa kutembea, kujenga na kushuhudia. Alipochaguliwa na Makardinali
wenzake, aliambiwa kamwe asiwasahau wala kuwatelekeza maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao n anafasi zao za maisha, ili kwamba wote
wanaotafuta: maana, huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, waweze kuuonja kwa
njia ya Mama Kanisa.
Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, dhamana ya uongozi
ni huduma kwa Taifa la Mungu pasi na kumezwa na malimwengu. Huruma na upendo wa Mungu
ambaye kamwe hachoki kusamehe na kusahau ni kati ya mambo makuu ambayo yameendelea
kukaziwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro, mwaka mmoja tangu achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki. Haya ni mambo ambayo
yameandikwa katika vinasaba vya maisha yake, kama inavyoonesha hata katika Nembo yake
ya Kipapa. Anasema upendo wa Mungu una nguvu ya kufanya mabadiliko makubwa katika
maisha ya mwanadamu. Kumbe, vijana wasikubali kamwe, kupokonywa matumaini ya maisha
yao na wajanja wachache.
Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Kanisa kutoka
Sakristia na kuwaendelea watu mahali waliko, ili waweze kuwaonjeshe huruma na upendo
wa Mungu kwa kuwatangazia Injili ya Furaha, huku wakikazia mambo msingi katika maisha.
Wachunguzi
wa masuala ya historia ya Kanisa walikuwa wanajiuliza maswali yasiyokuwa na majibu.
Je, inawezekanaje Kanisa kuwa na Mapapa mawili kwa mpigo? Baba Mtakatifu Francisko
ameonesha kwamba, jambo hili linawezekana hata pengine si mara ya kwanza kuanzia sasa
Kanisa likaweza kuwa na Papa mstaafu kama ilivyo kwa Papa mstaafu Benedikto wa kumi
na sita ambaye amekuwa kweli ni hazina ya Kanisa, Kiongozi mnyofu na asiyependa makuu
anayeutumia muda wake mwingi kwa ajili ya kutafakari Neno la Mungu na kuliombea Kanisa
la Kristo.
Baba Mtakatifu Francisko anawataka viongozi wa Kanisa kujitosa kimasomaso
kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu waliokabidhiwa kwao na Kanisa. Katika mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo, Kanisa halina budi kuwacha milango yake wazi kwa ajili
ya wote wanaotafuta kukutana na kuzungumza na Kristo; wale wanaotaka kujipatanisha
na Mungu pamoja na jirani zao; kwa wale wote wanaotaka kukumbatiwa na Mama Kanisa
ili kuondokana na upweke hasi unaowaandama katika hija ya maisha yao.
Baba
Mtakatifu Francisko anaendelea kulichangamotisha Kanisa kujenga na kudumisha utamaduni
wa kukutana na kujadiliana na watu kama sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wake.
Kanisa linatambua kwamba, lina dhamana ya kuganga na kuponya madonda mbali mbali yanayomwandama
mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani.
Watu waguswe na mahangaiko
ya jirani zao wanaoteseka kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, watu wasiokuwa
na ajira; watu ambao wamekumbwa na maafa asilia; watu wanaotaka kusalimisha maisha
yao kutokana na vita, dhuluma na nyanyaso za kidini na kikabila. Hili ni kundi la
watu ambalo linapaswa kumegewa na kushirikishwa udugu na mshikamano unaojali. Kwa
bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu kuna watu ambao kwa sasa vita, maafa ya wakimbizi
na wahamiaji huko Baharini si habari tena na wala hakuna anayetokwa na machozi kwa
watu kama hawa kufariki dunia.
Baba Mtakatifu anasema anaendelea kutekeleza
maamuzi yaliyotolewa kwenye Mabaraza ya Makardinali katika vikao vyao elekezi kabla
ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: Kwanza kabisa mageuzi haya hayana budi
kuanzia katika Sekretarieti ya Vatican, Benki ya Vatican pamoja na taasisi zote zinazoendeshwa
na Vatican kwa kukazia: weledi na huduma; nidhamu, ukweli na uwazi, kanuni pamoja
na sheria. Jambo la msingi ni toba na wongofu wa ndani.
Familia ni taasisi
ambayo kwa sasa inapewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko, ili kuhakikisha
kwamba, inaweza kutekeleza utume na dhamana yake kadiri ya mpango wa Mungu kwa maisha
ya mwanadamu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wajitaabishe kuhakikisha kwamba,
wanadumisha maagano ya Sakramenti ya Ndoa, pale ndoa inapovunjika, basi watu wasikitike,
kwani changamoto kubwa ni kuchuchumilia utakatifu wa maisha ya ndoa na familia.
Haki
na amani sehemu mbali mbali za dunia ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu anaendelea
kuyafanyia kazi kwa sala na majadiliano ya kina, lakini zaidi kwa kuitaka Jumuiya
ya Kimataifa kuwa makini na biashara ya silaha duniani inayoendelea kusababisha maafa
makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia. Baba Mtakatifu ni kati ya watu mashuhuri sana
duniani, lakini anayepaswa kupewa sifa na utukufu ni Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu.
Kwa ufupi haya ni kati ya yale yaliyojiri katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu
Francisko, Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, tarehe 13
Machi 2013.
Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Vatican.