Watu wengi wameguswa na kuvutwa na unyofu wa Papa Francisko
Mwaka mmoja umegota tangu Papa Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki.
Watu wengi ndani na nje ya Kanisa wamevutwa na kuguswa na maisha, ujumbe na changamoto
zinazoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu.
Ni ujumbe
na changamoto zinazogusa undani wa maisha ya mtu kwani zimesheheni: upendo na huruma
ya Mungu kwa watu wake. Ni kiongozi ambaye ameonesha ukaribu kwa watu maskini na wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kwa maneno mengine, huu ni upendo wa Mungu unaogusa
na kuponya.
Ni maneno ya Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican na
Mkurugenzi wa Radio Vatican, katika mahojiano maalum na Radio Vatican, wakati huu
Mama Kanisa anapomwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya Papa
Francisko, kutimiza mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Ni
mwaka ambao umekuwa na pilika pilika nyingi, lakini kuna matukio ambayo bado yanaendelea
kukumbukwa na wengi kwani yamenata katika mioyo ya watu kama nta safi. Moja kati ya
matukio haya ni usiku ule alipoinamisha kichwa chake, kuomba sala kutoka kwa maelfu
ya watu waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini
Vatican.
Padre Lombardi anakumbuka Alhamisi kuu jioni, alipowatembelea vijana
waliokuwa gerezani na kuadhimisha Ibada ya Misa ya Alhamisi kuu kwa kuwaosha miguu,
kielelezo cha huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Bado wengi wanamkumbuka Baba Mtakatifu alipofanya hija ya kichungaji Kisiwani Lampedusa
mlango wa matumaini ya watu kutoka Barani Afrika wanaopania kuokoa na kuboresha maisha,
wanapozama maji hata kabla ya kuwasili nchini Italia tayari kuelekea na safari zao
sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya.
Pengine maadhimisho ya Siku ya Vijana
Duniani kwa Mwaka 2013 yaliwagusa wengi kwani Baba Mtakatifu aliwapatia vijana changamoto
ya kutoa kipaumbele cha pekee kwa Kristo na Kanisa lake, wawe ni wadau wa Uinjilishaji
wa kina na wala si watazamaji wanaopunga upepo kutoka maghorofani!
Padre Lombardi
anasema, Waraka wa Injili ya Furaha ni muhtasari wa mpango mkakati wa shughuli za
kichungaji zinazopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya
Tatu ya Ukristo, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Familia ya Binadamu. Wazo hili
linajieleza wazi kutokana na Mabaraza ya Makardinali yaliyofanyika Mwezi Februari
2014 kwa kuangalia changamoto za kichungaji zinazoikumba Familia katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Padre Federico Lombardi
anasema kwamba, Kanisa ni Familia ya Mungu inayofanya hija ya toba na wongofu wa ndani,
tayari kujenga na kuimarisha Ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji;
ikiwa tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha ya mwanadamu.
Baba
Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Mwaka mmoja wa uongozi wake, ameendelea kulichangamotisha
Kanisa kufanya hija katika maisha na utume wake, kwa ajili ya mafao na maendeleo ya
binadamu wote, lakini zaidi wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Viongozi
wa Kanisa wawe makini kuonesha njia na dira kwa watu waliodhaminishwa kwao na Mama
Kanisa, ili waweze kuona barabara inayowaelekeza kwa Kristo na Kanisa lake. Hii ndiyo
hija inayofumbatwa katika Maadhimisho ya Sinodi mbali mbali zitakazoadhimishwa mjini
Vatican, kama kielelezo cha umoja, upendo na mshikamano wa Kikanisa. Haya ni mang’amuzi
ya kibinadamu na Kikristo.
Baba Mtakatifu Francisko ana mwono na mtazamo wa
mbali unaogusa maisha ya watu ndani na nje ya Kanisa. Anamwangalia binadamu aliyeumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu; anayepaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa tangu pale anapotungwa
mimba tumboni mwa Mama yake. Huu ndio ujumbe ambao Baba Mtakatifu anapenda kuwashirikisha
Wakuu wa Mataifa, Taasisi na vyombo vya habari wanapokutana na kuzungumza na Baba
Mtakatifu.
Kila mwamini anashirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Padre
Lombardi anasema, picha kubwa ambazo bado zinaendelea kuzunguka kichwani pake ni kuona
umati mkubwa wa watu wanaofurika kila Jumatano na Jumapili kwenye Uwanja wa Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican walau kumwona, kumsikiliza na kuzungumza naye.
Baba Mtakatifu kila mara anapohitimisha Katekesi yake, watu wa kwanza kusalimiwa ni
wagonjwa ambao hata katika mateso na mahangaiko yao, wanapendwa na kuthaminiwa na
Kanisa. Wagonjwa na maskini ni watu ambao daima wamekuwa na upendeleo wa pekee kutoka
katika Injili, jambo linalooneshwa pian a Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa.
Katika
sakata la habari kutoka mjini Vatican, mdau mkuu ni Baba Mtakatifu Francisko mwenyewe
anasema Padre Lombardi ambaye ndiye msemaji wake mkuu. Baba Mtakatifu ana uwezo wa
kuwafikia watu moja kwa moja bila hata ya kuhitaji huduma ya Msemaji mkuu wa Vatican,
jambo ambalo Padre Lombardi anasema, linamfurahisha sana. Ujumbe wa Baba Mtakatifu
unapaswa kuwafikia na kuwagusa watu moja kwa moja katika undani wao!
Imehaririwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.