Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kupokea salam na matashi mema kutoka katika Mabaraza
mbali mbali ya Maaskofu, viongozi wa Serikali pamoja na watu binafsi kwa kutimiza
Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki hapo tarehe 13 Machi 2013.
Tangu wakati huo Kanisa likaanza utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji
kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii
pamoja na Familia ya binadamu katika mwanga wa Injili ya Kristo. Utu na heshima ya
mwanadamu vimeendelea kupewa umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Mama Kanisa,
kwa njia ya ushuhuda wa unyenyekevu na maisha manyofu ynayooneshwa na Papa Francisko.
Lengo ni kumwonjesha binadamu huruma na upendo wa Mungu.
Hivi ndivyo anavyosema
Askofu mkuu Joseph Edward Kurtz, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani katika
salam na matashi mema kutoka katika Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, wakati huu
Baba Mtakatifu anapoadhimisha Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki.
Amekuwa ni mfano bora wa kuigwa na viongozi wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake.
Ni kielelezo bora cha kuigwa katika maisha na utume: kama Mchungaji, Padre
na kama Kiongozi Mkatoliki, lakini zaidi kama binadamu. Baba Mtakatifu amesaidia kuleta
nguvu na mwamko mpya kwa viongozi wa Kanisa na waamini katika ujumla wao; amekazia
na kuhimiza Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayojikita katika: maisha, utu na heshima
ya binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko ameonesha kipaumbele cha pekee kwa Familia
na changamoto zake ili kukabiliana na changamoto hizi za kichungaji, huku Kanisa likiwa
limeshikamana katika umoja na udugu. Kanisa linapenda kuangalia wapi ambako ni chimbuko
la matatizo ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo, kwani kuanguka kwa tunu
msingi za maisha ya ndoa na familia ni kuporomoka kwa Jamii nzima ya mwanadamu. Kwa
kutoa kipaumbele cha pekee kwa maisha ya ndoa na familia ni kutaka kuwajengea watu
matumaini mapya katika maisha yao, licha ya magumu na majanga wanayokumbana nayo!
Kwa
upande wake Kardinali Oswald Gracias, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki India anasema,
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulichangamotisha Kanisa kutoa kipaumbele cha
pekee katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, Umuhimu wa Mafundisho Jamii ya Kanisa,
Neno la Mungu linalopaswa kutangazwa kwa furaha na bashasha kubwa na wala si kama
watu walionjeshwa pilipili kichaa!
Umoja, usawa na udugu ni changamoto kuu
zinazopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko. Jimbo kuu la India, linaendelea
kumuenzi Baba Mtakatifu kwa Ibada ya Misa Takatifu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu,
ili aweze kufanikisha nia njema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.
Mjini
Assisi, Wafranciskani kwa namna ya pekee wanaendelea kumwimbia Mungu utebnzi wa sifa
na shukrani kwa Baba Mtakatifu Francisko kumuenzi Mtakatifu Francisko wa Assisi katika
maisha na karama yake kwa ajili ya Kanisa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Ufukara wa Kiinjili, Amani na Utunzaji bora wa mazingira ni mambo muhimu katika ulimwengu
unaoendelea kukabiliwa na maafa mbali mbali. Katika mambo yote, Yesu, Kanisa na Mwanadamu
wapewe kipaumbele cha kwanza.
Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.