Wakristo wanachangamotishwa na Mama Kanisa kujitokeza kifua mbele kuwatangazia watu
Injili ya Furaha na kuwaonjesha ushuhuda wa imani tendaji inayofumbatwa katika Neno
la Mungu na maisha ya Kisakramenti. Kuna maelfu ya wakristo ambao wamesahau Mlango
wa Kanisa, hawa wanapaswa kuoneshwa ushuhuda wa maisha ya Kikristo yenye mvuto na
mashiko.
Wakati wa
kupepeta mdomo umekwisha, watu wanataka kuona Injili ikilimwilisha katika uhalisia
wa maisha ya watu, vinginevyo watu wataendelea kuogelea katika utupu na mkanganyiko
wa maisha. Wakristo wajitokeze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji
Mpya unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa kuwashirikisha watu Injili
ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Hii ni changamoto
ambayo imetolewa hivi karibuni na Kardinali Antonio Canizares Llovera, Mwenyekiti
wa Baraza la Kipapa la Ibada na nidhamu ya Sakramenti, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu
kuhitimisha Jubilee ya Miaka 100 tangu Jimbo la Bikira Maria wa Antiqua lilipoanzishwa.
Itakumbukwa kwamba, hili ni Jimbo la kwanza kabisa kuanzishwa Amerika ya Kusini.
Kardinali
Canizares Llovera alikuwa anamwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika kufunga Jubilee
hii ambayo ilizinduliwa Mwezi Septemba 2012, kwa mwaliko wa kumwilisha Injili ya
Furaha katika vipaumbele vya maisha ya waamini, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani
tendaji. Waamini hawana sababu ya msingi ya kuogopa “kujimwaga duniani” kwa ajili
ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Furaha, huku wakiendelea kuwamegea jirani zao
upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Waamini wawe ni watu
wenye uwezo wa kupokea na kutoa msamaha kwa wale wanaowakosea, dhamana ambayo kimsingi
si lele mama kutokana na ukweli kwamba, watu wengi wanapenda kulipiza kisasi. Wakristo
wawe ni chombo cha upendo kwa watu wanaoteseka kutoka na umaskini, ujinga na maradhi.
Wawe ni kielelezo cha matumaini ya watu waliokata tamaa kutokana na umaskini wa kiroho,
unaotaka kumng’oa Mungu kutoka katika undani wa maisha na mikakati yao.
Kardinali
Canizares Llovera anawaonya waamini kutoyakumbatia malimwengu, bali wawe ni chumvi
na mwanga wa kuyatakatifuza, kwa kuonesha ukomavu katika uhuru na ushuhuda wa imani
tendaji. Hapa hakuna Injili Mpya inayotangazwa, bali ni umwilishaji wa Neno la Mungu
ili kuyachachua malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayojikita katika imani
kwa Kristo na Kanisa lake. Kardinali Antonio Canizares Llovera anahitimisha mahubiri
yake kwa kuwaweka Wakristo wote wa Panama chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria,
msimamizi wao, ili awasaidie kuwa kweli ni cheche za matumaini kwa Familia na kwa
nchi ya Panama katika ujumla wake.