Miaka 30 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Marekani
Vatican na Serikali ya Marekani mwaka 2014 kwa pamoja wanaadhimisha kumbu kumbu ya
miaka 30 tangu Marekani ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican, hapo tarehe
10 Januari 1984. Rais mstaafu Ronald Reagan alitangaza mchakato wa kuanzisha uhusiano
wa kidiplomasia na Vatican. Tarehe 8 Machi 1984, Serikali ya Marekani ikatuma Balozi
wake wa kwanza mjini Vatican. Tarehe 26 Machi 1984 Mwenyeheri Yohane Paulo II akamteuwa
wakati huo Askofu mkuu Pio Laghi kuwa ni Balozi wa kwanza wa Vatican nchini Marekani.
Wachunguzi
wa mambo ya kisiasa wanasema, si bure kwamba, Rais Barack Obama wa Marekani ameamua
kutembelea Vatican ili kukutana na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 27 Machi 2014
wakati wa ziara yake ya kikazi Barani Ulaya Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais
Obama kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Viongozi hawa wawili wanakubaliana
kimsingi katika agenda moja ya kupambana kufa na kupona na umaskini, ili kujenga mshikamano
wa kidugu kati ya watu.
Katika kipindi cha miaka thelathini ya uhusiano wa
Kidiplomasia kati ya Vatican na Marekani, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika majadiliano
na mchango wa nchi hizi mbili katika medani za Jumuiya ya Kimataifa. Tangu mwaka 1984
hadi kufikia mwaka 2014, Marekani imekwishatuma Mabalozi wake kumi kama wawakilishi
wa Serikali ya Marekani mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, tarehe 21 Oktoba 2013 Bwana
Kenneth Francis Hackett, Balozi wa Marekani mjini Vatican aliwasilisha hati zake za
utambulisho kwa baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.
Huyu ni mwanasiasa
ambaye kwa miaka mingi amekuwa ni Makamu wa Rais wa Shirika la Misaada la Baraza la
Maaskofu Katoliki Marekani, Mjumbe wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa
Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis. Kuanzia mwaka 1994 hadi kufikia mwaka
2012 alikuwa pia ni mjumbe wa Shirika la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki,
Cor Unum. Ni matumaini ya Balozi Kenneth Francis Hackett kwamba, Marekani na Vatican
wataendelea kushirikiana kwa karibu zaidi kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo
ya Jumuiya ya Kimataifa.