2014-03-12 08:50:11

Angalieni msije mkatekwa na kumezwa na malimwengu!


Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu. Anaonesha ukuu na utakatifu wa maisha ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Maisha ya mwanadamu yanaweza kuwa hatarini ikiwa kama, watu hawataruhusu huruma na upendo wa Mungu kupenyeza hadi kwenye undani wa maisha ya mwanadamu, kwa kushikamana katika umoja na upendo.

Huu ni muhtasari wa tafakari ya Mafungo ya Kiroho yanayotolewa na Monsinyo Angelo De Donatis, kwa Baba Mtakatifu Francisko na wasaidizi wake wa karibu wakati huu wanapoendelea na Mafungo ya Kipindi cha Kwaresima huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma. Anasema mwanadamu anakabiliwa na dhambi inayotaka kumteka na kummiliki mwanadamu kama ilivyokuwa kwa yule Mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu katika mji wa Dekapoli na makao yake makuu yalikuwa ni makaburini.

Yesu anaonesha nguvu zake kwa kumwokoa yule kijana na pepo wachafu na hivyo kuanza tena hija ya maisha yake ya kawaida. Wananchi wa Dekapoli wao waliguswa zaidi na masuala ya kiuchumi kwa kupoteza Nguruwe wao elfu mbili, wakashindwa kukutana na Yesu Mkombozi wa ulimwengu. Yesu anaendelea kushinda mapepo ya sera za kiuchumi zinazotaka kummiliki mwanadamu ili kufisha uwezo wake wa kukutana na Mwenyezi Mungu. Yesu anataka kumwokoa mwanadamu kutoka katika woga, hofu na mashaka, kwa kumwonjesha huruma na upendo wa Mungu.

Monsinyo Angelo De Donatis anasema, ili kuweza kuonja huruma na upendo wa Mungu kuna haja kwa mwamini kuomba msaada na nguvu ya Roho Mtakatifu, ili kutambua mambo msingi katika maisha sanjari na kukumbatia upendo na huruma ya Mungu inayofumbatwa katika maisha ya Yesu. Kumbe kuna uhusiano wa pekee kati ya matendo ya mwanadamu na neema ya Mungu. Si jukumu la Kanisa kuwaonesha walimwengu mambo ambayo yanafanywa na Mapadre, Watawa na Waamini walei ndani ya Kanisa, bali kuonesha kazi ya Mungu inayotendwa kwa njia ya watu wake.

Monsinyo De Donatis anasema, hapa Mwenyezi Mungu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala si kazi wala mikakati ya Kanisa, vinginevyo wanaweza kumezwa na malimwengu. Waamini watambue kwamba, ni wadhambi waliosamehewa dhambi zao kwa njia ya neema ya Mungu na wala si kwa sheria kama anavyosema Mtakatifu Paulo katika Nyaraka zake. Katika ulimwengu wa utandawazi kuna kishawishi kikubwa cha watu kutaka kuonekana mbele ya Jamii kwa yale wanayotenda, lakini Yesu Kristo anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika matendo mema.

Wakristo wanaalikwa kuchunguza dhamiri zao kwani ni baadhi ya watu hata baada ya kuona matendo makuu ya Mungu yanayofanywa na Kanisa bado wanashikwa na kigugumizi cha kumshurukuru, kumtukuza na kumsifu Mwenyezi Mungu? Hapa kuna jambo ambalo haliendi vyema anasema Monsinyo De Donatis. Mikakati ya shughuli za kichungaji inapaswa kuwa kweli ni matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu, lakini kwa bahati mbaya, leo hii viongozi wengi wa Kanisa wanajitaabisha mno kufanya mambo mengi katika shughuli za kichungaji.

Waamini wanakumbushwa kwamba, matunda ya imani ni matokeo ya mwamini kukutana na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yake. Ndivyo anavyokazia Monsinyo Angelo De Donatis katika mahubiri yake kwa Baba Mtakatifu Francisko na wasaidizi wake wa karibu.







All the contents on this site are copyrighted ©.