Mshikamano na umoja wa kitaifa ili kupambana na changamoto mbali mbali nchini Togo!
Baraza la Maaskofu Katoliki Togo katika ujumbe wake mara baada ya maadhimisho ya mkutano
wake mkuu linasema kwamba, mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Ukweli, Haki na Amani,
kuhusu mchakato wa uchaguzi mkuu na mabadiliko msingi yanayopaswa kufanywa kwenye
Serikali pamoja na taasisi zake, yanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha msingi
ya haki na amani; utawala bora unaozingatia sheria pamoja na kukoleza maendeleo na
mafao ya wengi.
Maaskofu Katoliki nchini Togo pamoja na mambo mengine wamejielekeza
zaidi katika masuala nyeti na changamoto zinazoendelea kuwaandama wananchi wa Togo
katika ujumla wao. Maaskofu wanaitaka Serikali, vyama vya kisiasa na wadau wengine
kujikita katika mchakato wa upatanisho, haki na amani ambao umezinduliwa hivi karibuni
nchini humo.
Maaskofu wamejadili pia umuhimu wa majiundo makini na endelevu
kwa ajili ya Mapadre na Watawa nchini Togo, bila kusahau kuwajengea uwezo walei na
wanasiasa ili kutekeleza wajibu wao msingi katika maendeleo na ustawi wa wananchi
wa Togo.
Baraza la Maaskofu limeangalia pia maisha na utume wa Kanisa Katoliki
nchini Togo, ambalo waamini wake ni zaidi ya asilimia ishirini ya idadi yote ya wananchi
wa Togo. Maaskofu wanajiandaa kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika matukio mbali
mbali ya maisha ya Kanisa la Kiulimwengu na kwa namna ya pekee, sherehe za kuwatangaza
Wenyeheri Yohane wa XXIII na Yohane Paulo II kuwa ni watakatifu hapo tarehe 27 Aprili
2014.
Maaskofu wamegusia mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya huduma,
majiundo awali na endelevu, mafundisho ya dini shuleni, hija za maisha ya kiroho ndani
na nje ya Togo pamoja na kufanya mabadiliko katika Mahakama ya Kanisa Katoliki nchini
kwa kuangalia kwa makini masuala ya kijamii na kisiasa nchini humo. Ni jukumu la wananchi
wa Togo kushikimana na kujenga utawala wa sheria unaozingatia haki msingi za binadamu,
umoja wa kitaifa, upatanisho na maendeleo endelevu.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Togo limeweka Mpango wa shughuli za kichungaji mwa kipindi cha Miaka mitatu, kwa kutoa
kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii. Itakumbukwa
kwamba, kunako miaka 1990 Togo ilijikuta inatumbukia katika mgogoro wa kisiasa na
kiuchumi, hali iliyopelekea wananchi wengi kutumbukia katika umaskini wa hali na kipato.
Hadi sasa kuna idadi kubwa ya wananchi wa Togo wanaishi chini ya kiwango cha umaskini
duniani.