2014-03-11 12:13:37

Mali ya watawa ni kwa ajili Unjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili!


Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume hayana budi kuhakikisha kwamba, yanatumia vyema mali ya Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa katika maeneo yao, huku wakisukumwa na fadhila ya huduma ya upendo kwa wale wanaowahudumia. Hii ni huduma ya upendo inayodhihirisha imani tendaji katika maisha ya watu.

Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa Ibada ya Masifu ya Jioni kwa ajili ya watawa waliokuwa wanashiriki katika semina maalum kwa ajili ya wasarifu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Semina hii ya kimataifa ya siku tatu ilikuwa imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume na ilifanyika kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Antoni kilichopo mjini Roma. Watawa wamekumbushwa kwamba mali waliyo nayo ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu na utume wa Kanisa.

Kardinali Parolin anasema, Yesu alipokuwa anajaribiwa Jangwani alimwambia Shetani kwamba, mtu hataishi kwa mkate peke yake bali kwa kila neno linalotoka kinywani mwa Bwana. Huu ni mwaliko kwa watawa kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema rasilimali na mali waliyokabidhiwa na Mwenyezi Mungu kwa hekima na busara; katika ukweli na uwazi; huku wakiwajibika barabara. Mashauri ya Kiinjili yajidhihirishe wazi katika matumizi bora ya mali zinazomilikiwa na watawa pamoja na kupambanua kikamilifu vipaumbele vya matumizi ya mali hii.

Wakati huu wa athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kuna haja kwa watawa kujifunga kibwebwe kuhakikisha kwamba, karama ya mashirika yao inakuwa ni kigezo msingi katika kuchagua vipaumbele vya matumizi ya mali ya Mashirika ya Kitawa. Wachunguze kwa umakini mkubwa wapi ambapo kumekuwepo na uzembe kiasi kwamba, Mashirika haya yamepoteza mali ya Kanisa au mali hii imetumika kinyume cha taratibu na kanuni za Shirika husika.

Kardinali Parolin anasema, inasikitisha kuona kwamba, athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinaathiri hata utendaji wa shughuli za huduma msingi kwa Jamii katika nchi za Kimissionari. Ili kukabiliana na changamoto hizi zote, watawa wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanaongozwa vyema na Neno la Mungu linalomwilishwa katika karama na moyo wa Shirika katika utimilifu wake.

Wasi wasi wa athari za myumbo wa uchumi kimataifa zisiwafanye watawa kutowashirikisha wengine huduma ya upendo kwa kama walivyohofia Mitume walipokuwa kule Jangwani wakajikuta wakiwa na Samaki watano na Mikate miwili, lakini Yesu kwa njia ya ukarimu huu aliweza kuwalisha watu zaidi ya elfu tano kama inavyosimuliwa katika Injili.

Mashirika ya kitawa yajifunze kubana matumizi, lakini yawe pia na mbinu na mikakati ya matumizi bora ya mali ya Shirika. Watu wanaokabidhiwa kutunza fedha na mali ya Shirika waandaliwe vyema, kwa kutambua kwamba, mali hii ni kwa ajili ya huduma ya Kiinjili inayomwilishwa katika upendo kwa ajili ya Mungu na mwanadamu. Watawa wakiweza kudhibiti matumizi ya fedha na mali ya Mashirika yao kwa ajili ya huduma kwa Kanisa, wataweza kushangaa kuona kwamba, fedha na mali hiyo inaongezeka maradufu.

Hakuna muujiza ambao Mwenyezi Mungu anaweza kuufanya kwa kuongeza fedha na mali ya Mashirika ya Kitawa, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa, wanatumia vyema fedha na mali ya Mashirika kwa malengo yaliyowekwa mintarafu karama ya Shirika husika, huku wakiendelea kuwa na matumaini kwa Mwenyezi Mungu badala ya kujikatia tamaa na kujifunga katika ubinfasi na uchoyo wao.

Kardinali Parolin anawaambia Watawa kujitahidi kwanza kuutafuta Ufalme wa Mungu na mengineyo watayapata kwa ziada. Kwa kuwa na matumizi bora ya rasilimali na mali ya Mashirika ya Kitawa, kazi ya Uinjilishaji Mpya itasonga mbele.

Akichangia mada kwenye semina hii ya kimataifa, Kardinali Joao Braz de Avis, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume amewataka watawa kuwa na matumizi bora na sahihi ya mali ya Mashirika. Viongozi wa Mashirika wamepewa dhamana na Kanisa kusimamia na kuratibu mali ya Mashirika kwa kusaidiana na Wasarifu wao.

Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, matumizi ya mali na fedha za Mashirika ya Kitawa yanafuata Sheria na Kanuni za Kanisa na Mashirika husika, ili kudhibiti ubadhirifu unaoweza kufanywa na baadhi ya watawa wanaoweza kumezwa na malimwengu na hivyo kusababisha kashfa kama ambavyo zimewahi kujitokeza ndani ya Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Mali ya Kanisa inapaswa kudhibitiwa na Sheria pamoja Kanuni za Kanisa pamoja na Sheria za nchi husika.

Washiriki wa semina hii ya kimataifa wamegusia pia matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa mikakati mbali mbali ya kichungaji kwa ajili ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kimsingi, imesisitiziwa kwamba, Sheria, Kanuni na Katiba za Mashirika katika matumizi ya mali za Kanisa zinapaswa kufuatwa kikamilifu bila kupuuziwa hata kidogo.







All the contents on this site are copyrighted ©.