Mafungo ni kipindi cha kufungua moyo ili kumsikiliza Roho Mtakatifu
Utakaso wa roho ndiyo kauli mbiu inayoongoza Mafungo ya kiroho ya Baba Mtakatifu Francisko
pamoja na wasaidizi wake wa karibu yaliyoanza tangu Jumapili jioni huko Ariccia, nje
kidogo ya mji wa Roma. Mafungo haya yanaongoza na Monsinyo Angelo De Donatis, Paroko
wa Parokia ya Mwinjili Marko, Jimbo kuu la Roma.
Baba Mtakatifu wameendelea
kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu, Tafakari na Ibada ya Kuabudu Ekaristi
Takatifu. Monsinyo De Donatis katika tafakari yake anaendelea kukazia umuhimu wa mafungo
katika maisha ya mwamini, changamoto kwao ni kujifunua kwa Roho Mtakatifu, ili kuimarisha
maisha ya kiroho yanayowasaidia kukutana na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao
ya ndani, wakiwa na mwanga mpya unaotoka kwa Mwenyezi Mungu.
Mafungo haya yawasaidie
kukuza moyo wa: Sala, Ibada na Majitoleo kwa Mwenyezi Mungu pamoja na Kanisa lake.
Ni wajibu wa waamini kutambua uwepo wa Mungu katika kazi ya uumbaji, bila ya kumwogopa.
Itakumbukwa kwamba, wakati fulani katika maisha yao, mitume walishikwa na woga, kwa
sababu hawakuwa na imani thabiti. Hali hii inaweza kumkuta mwamini ikiwa kama hawezi
kuzamisha uhusiano wake wa dhati na Yesu Kristo na kusahau kwamba, Mwenyezi Mungu
ni mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake.
Ukosefu wa imani anasema Monsinyo
De Donatis kwamba, waamini wanajikuta wakiogelea katika maisha ya kinafiki na kutokujali,
hali inayomfanya mhusika kutoa amri bila ya yeye mwenyewe kujihusisha katika utekelezaji
wake. Ni watu wanaotaka kuwabebesha wengine mizigo mizito bila yao wao wenyewe kushiriki.
Kumbe,
kuna haja kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanasafisha roho zao ili kuondokana na picha
hasi ya uwepo wa Mungu katika maisha yao, ili kuanza mchakato wa maisha ya kweli na
matakatifu pasi na mawaa!