Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, karibu tena katika kipindi chetu cha Kanisa
la nyumbani. Tukiwa ndani ya Kipindi cha Kwaresma, tunaendelea kuitikia mwito wa kumrudia
Mungu atualikaye akisema “nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote kwa maana mimi ni mwenye
rehema na upole”.
Katika kipindi
hiki ambapo tunashughulikia kwa namna ya pekee zaidi wongofu wa mwenendo wetu, tunakiri
udhaifu wetu mbele za Mungu na mbele za wanadamu wenzetu, na hivyo kwa roho ya unyenyekevu
toba na majuto ya kweli, tunataka kurekebisha yale yote yanayotuweka mbali na Mungu
wetu na pia yanayotutenga na wanadamu wenzetu. Kipindi cha Kwaresma ni kipindi cha
Kusali sana, kutoa sadaka na kufunga.
Mpendwa msikilizaji, kwa siku ya leo,
tuone kwa ufupi juu ya tunu hii ya sala katika maisha yetu ya kila siku. Sisi sote,
kila mmoja kwa nafsi yake, anautafakari na kuukiri wema na ukuu wa Mungu. Lakini
kwa udhaifu wetu sisi wenyewe na kwa hila za yule mwovu, hatujafaulu sana kumpa Mungu
utukufu. Daima tunamsahau Mungu, ila Mungu hatusahau kamwe, anasikitika pale tunapomkimbia
kwa maisha yetu ya dhambi, na ndiyo maana anatuita akisema “nirudieni mimi kwa mioyo
yenu yote”. Sio tunarudi kwa mashakamashaka au tunamrudia kwa kujaribisha au kukejeli,
ila asema nirudieni kwa mioyo yenu yote.
Katika kipindi hiki cha Kwaresma,
tunataka kuongea na Mungu zaidi, kutafakari wema wake wa kila siku na kuukiri ukuu
na uweza wake kwa maneno na matendo ya maishani mwetu. Tunafanya hivyo kwa njia ya
sala na tafakari. Lakini sala yetu ili ipate kibali mbele za Mungu lazima iwe nadhifu
na kunjufu. Sala nadhifu ni ile ambayo ina nia njema na inaendana na hulka ya Mungu
mwenyewe, yaani upendo, wema, upole huruma, uaminifu na uvumilivu. Hatuwezi kumkejeli
Mungu kwa kumwomba atusaidie tufanikiwe katika maovu, au kumwomba awatendee maovu
wenzetu, hiyo siyo hulka ya Mungu. Sala kunjufu ni sala yenye nguvu ya kinabii, ni
sala inayompa Mungu Utukufu na kumtakatifuza mwanadamu. Tunaalikwa kusali kwa nidhamu
ya akili, mwili na roho.
Bwana asema “tena msalipo, msiwe kama wanafiki,
maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia
ili waonekane na watu. Amini nawaambia wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo,
ingia katika chumba chako cha ndani, na ukisha kufunga mlango wako usali mbele ya
baba yako aliye sirini atakutuza” (Mt. 6-6). Neno hili litukumbushe sote
juu ya unadhifu wa sala zetu. Tunaalikwa kukwepa kabisa kishawishi cha nyakati zetu
hizi cha kupenda kusali kwa matamasha na TV, ili tuonekane na watu na kuyapendezesha
macho ya watu badala ya kuupendezesha moyo wa Mungu. Siku zetu hizi kuna kishawishi
cha kusali kwa kelele nyingi za viigizo, na kurukaruka kwingi, badala ya kusali kwa
ibada na tafakari. Kusali kwa aina hiyo hakuna thawabu machoni pa Bwana. Sala ya kweli,
hutoka katika vilindi vya mioyo yetu, nayo hufanyika katika utulivu. Mungu wetu, sio
Mungu wa kelele.
Na tena, Neno la Mungu latukumbusha kusali kila wakati. Tunakatazwa
kusali kwa matukio au kwa msimu tu. Neno anasema “Salini daima, mkiomba msaada wa
Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili
ya watu wote wa Mungu (Ef. 6:18) na pengine asema, salini kila wakati na kushukuru
katika kila jambo (1Thes 5:17-18).
Neno hili ‘salini kila wakati’, na likae
mioyoni mwetu kipindi hiki cha kwaresma na nyakati zote. Mpendwa msilikizaji, ikumbukwe
kwamba Mungu wetu sio Mungu wa matatizo. Huweza kutokea kwa baadhi yetu, tukawa watu
wa kusali pale tu tupatwapo na matatizo. Yaani matatizo yanakuwa ndiyo teke la kutukumbusha
juu ya uwepo wa Mungu na umuhimu wa sala. Tukipatwa na shida, ndio tunamkumbuka Mungu.
Katika mazingira hayo, hiyo inakuwa sio sala bali ni kelele za kumsimulia Mungu matatizo
yetu. Imani ya matatizo haina thawabu mbele za Bwana.
Mpendwa msikilizaji,
sasa tuielekeze tafakari yetu katika familia zetu. Uhalisia unashuhudia kwamba, familia
nyingi zimeacha kuwa shule ya sala. Baba Mtakatifu Francisco mara nyingi ameonesha
sikitiko juu ya ukosefu wa sala katika familia, ambapo wazazi na wote wenye dhamana
ya malezi, wamesahau kuwafundisha watoto sala, hata ishara ya msalaba tu inakosekana.
Dini gani hiyo isiyokuwa na sala? Ni muamini wa aina gani huyo asuifahamu sala za
dini yake? Kwaresma hii tukumbushwe tena, familia ni shule ya sala. Tuwafundishe watoto
wetu KUSALI. Nasi sote tujibidishe kufahamu sala na namna ya kusali.
Familia
iwe ni kanisa linalosali! Ukweli unashuhudia kwamba, familia nyingi zimeacha kusali
pamoja. Hatuwezi kusingizia sana utandawazi, bali namna yetu ya kupima mambo kwa vipaumbele.
Kuna mambo mengi sana ambayo familia hufanya pamoja, lakini ugonjwa mbaya wa kiroho
umeingia katika familia nyingi, hawawezi kusali pamoja tena. Tunakumbushwa wanafamilia,
tukutanike pamoja, tuliite jina la Bwana pamoja, tulitaje jina la Mungu wetu kwa pamoja
(Zab 34:1-7). Kulitaja jina la Bwana kwa pamoja kama familia kuna maana na uzito wake.
Kuwa na utengano katika sala, yule mwovu anaweza kukujaribu vibaya mno, ndipo
hapo mtu unapopata kishawishi cha kumwombea mabaya mwenzako (mama unamwombea baba
apatwe na mabaya, na baba unamwombea mama maangamizi), lakini mngesali kwa pamoja,
nyote mngetamka, utupe leo mkate wetu wa kila siku.
Kipindi hiki cha kwaresma
tunataka kupiga vita roho ya uvivu katika sala inayoelekea kuota mizizi mirefu sana
katika familia zetu. Tunataka pia kupiga vita roho ya kuionea aibu sala. Wengi wanaona
aibu kusali. Imani yetu bila sala, itanyauka na kufa kabisa na mwovu anapata nguvu
ya kutupepeta apendavyo.
Sala inatupatia nguvu ya ndani ya kustahimili
mitikisiko ya maisha. Sala inatuliza akili zetu wakati wa mahangaiko. Sala inatupatia
ujasiri wa ajabu hata mbele ya matatizo makubwa. Sala inatupatia amani hata kama tunapita
motoni na majini. Sala ni mlango wa tumaini jema daima. Sala ni afya ya roho na ya
mwili. Tusali daima kwani kusali ni heri.
Kutoka katika studio za Radio
Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.