Sala Maalum kwa ajili ya Kuombea Bunge Maalum la Katiba Tanzania
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anawaalika
waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea Bunge Maalum
la Katiba linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma. Ifuatayo ni sala unayoweza pia
kuwashirikisha jirani zako:
Bwana Yesu, Ulizaliwa Pangoni Bethlehem wakati
Yosefu na Maria walipokwenda kusajili majina yao kwenye kitabu cha orodha ya raia.
Nawe unaelewa umuhimu wa uongozi na utawala bora wa kiraia.
Nasi, wananchi
wa Tanzania, sasa tupo katika kipindi muhimu kwa historia yetu. Wakati huu tunatafuta
kwa pamoja namna ya kuendesha jamii yetu na kuweza kuboresha miundo yetu na taratibu
zetu. Ee Bwana Yesu tunaomba msaada wako.
Utujalie mwanga wa Roho Mtakatifu
na uvuvio wake, ili tuweze kutumia busara na hekima katika kutafuta yaliyo mema kwa
taifa letu na mustakabali wake. Kwa namna ya pekee tunakuomba waangazie na kuwapa
hekima wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba, ili mioyo yao ijazwe upendo wako ulio
nao kwa Taifa letu na watu wake. Tunawaombea waweze kuepuka kufanya kazi hiyo kwa
kuongozwa na maslahi binafsi ama kutawaliwa na mawazo finyu ambayo ni kwa maslahi
ya kisiasa tu.
Tunakusihi, tawala mioyo yao wakati wote wa mijadala wazingatie
yaliyo mema kwa nchi yetu na watu wake.
Kwa Maombezi ya Bikira Maria, tunakuomba
utongoze katika wakati huu muhimu kwa nchi yetu. AMINA.
Sala hii imetiwa sahihi
na Askofu Tarcisius J. M. Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
na Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa Tarehe 02. 03. 2014.