2014-03-10 08:30:05

Kwaresima kiwe ni kipindi cha kusaidia mchakato wa utunzaji bora wa mazingira


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa, akizungumza na Waandishi wa Habari waliokuwa wamefurika mjini Vatican kufuatilia mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, alisema amechagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assis, kwani alikuwa ni mtu fukara, mpenda amani na mazingira. RealAudioMP3

Hii ndiyo changamoto inayofanyiwa kazi katika Kipindi hiki cha Kwaresima na Baraza la Maaskofu Katoliki India, kuhakikisha kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanashirikishwa katika kulinda na kutunza mazingira. Waamini wanahimizwa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kama sehemu ya ushiriki wao katika kulinda na kuendeleza kazi ya Uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu ili aweze kutunza kwa ajili yake na kwa kizazi kijacho.

Kardinali Oswald Gracias, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki India anasema, Kipindi cha Kwaresima: muda wa kusali na kufunga, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu kama kielelezo cha imani tendaji katika matendo ya huruma, iwe ni fursa ya kujenga na kuimarisha uhusiano mwema kati ya mwanadamu na Muumba wake pamoja na mazingira.

Uharibifu wa mazingira ni kati ya changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa India kwa sasa. Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya viwanda na uzalishaji; mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira. Kanisa kwa nyakati zote limekuwa ni mdau mkubwa wa utunzaji wa mazingira, kumbe halitaweza kukaa pembeni na kuona mazingira yakiharibiwa.

Jimbo kuu la Bombay, India, hivi karibuni lilianzisha Idara ya Mazingira ili kuweza kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari zake. Katika kipindi hiki cha Kwaresima, Idara ya mazingira inaendelea kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi na ustawi wa wananchi wote wa India na dunia katika ujumla wake.








All the contents on this site are copyrighted ©.