Kardinali Chibly Langlois wa Jimbo Katoliki la Les Cayes, kutoka Haiti aliyeteuliwa
na kusimikwa hivi karibuni wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu
Petro, Jumapili tarehe 9 Machi 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ili kumshukuru
Mungu kwa kuteuliwa kuwa ni Kardinali wa kwanza kutoka Haiti, changamoto ya kuonesha
mshikamano wa umoja, upendo na udugu kwa wote.
Waamini wa Kanisa Katoliki
nchini Haiti wametumia fursa hii kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko,
amani, utulivu na upendo wakati huu anapoadhimisha Kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu
alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Kardinali
Langlois katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu iliyodumu kwa takribani
masaa matatu, amewataka wananchi wa Haiti katika ujumla wao, kujenga na kuimarisha
mshikamano wa upendo ili kuwasaidia wale ambao wanaendelea kuteseka kutokana na baa
la njaa, umaskini na ujinga nchini Haiti. Watoto wengi wameweza kwenda shule, kupata
chakula na makazi bora kutokana na mchango wa Wasamaria wema.
Huu ni mwaliko
kwa wananchi wote wa Haiti kushikamana kidugu ili kusaidiana kupambana na changamoto
za maisha ya kila siku. Waamini na wananchi katika ujumla wao, wawe na ujasiri wa
kushirikisha hata kile kidogo walicho nacho kwa ajili ya mafao ya wengi.
Kardinali
Chibly Langlois mwenye umri wa miaka 55 ambaye ni kati ya Makardinali wenye umri mdogo
kwenye Baraza la Makardinali anaonesha jinsi ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyowathamini
na kuwajali watu wanyonge, ili waweze kuondokana na unyonge wao, tayari kutoka kifua
mbele kuwatangazia jirani zao Injili ya Furaha. Hata maskini katika umaskini wake,
bado ni sehemu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa linataka kuwahudumia
maskini kwa ari na moyo mkuu kama anavyoonesha Baba Mtakatifu Francisko katika maisha
na vipaumbele vyake.
Kardinali Langlois katika mahubiri yake amekazia pia umuhimu
wa wananchi wa Haiti kushikamana kwa dhati, ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa.
Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa pia na watu wa dini na madhehebu mbali mbali
nchini Haiti kwa kutambua kwamba, Kardinali Chibly Langlois ameteuliwa si tu kwa ajili
ya Kanisa Katoliki nchini Haiti, bali ni daraja la upendo kwa watu wote.
Ibada
hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Uwanja wa michezo wa Port - au Prince- kwani
Kanisa kuu la Jimbo kuu la Port- au- Prince lilibomoka wakati wa tetemeko la ardhi
lililoikumba Haiti kunako Mwaka 2010 na bado halijaanza kujengwa tena.