2014-03-08 15:11:09

Jichungulie mwenyewe!


Kwa mara nyingine tena tunabahatika kukiingia kipindi maarufu cha Kwaresima, kipindi cha sala, kipindi cha upambanuzi wa maisha binafsi na cha wongofu. Kwa dhati tunaweza kusema kuwa kwaresima ni wakati wa kujikuta, kujitambua na wa kujielewa jinsi nilivyo mimi binafsi na uhalisia wa jinsi nilivyo mimi binafsi kuliko kusema ni kipindi cha kujitesa.

Kwa hiyo, siyo tu kipindi cha kufanya tendo pekee la upendo au la kujitesa, la hasha, bali pia ni kipindi cha kuufahamu ukweli wangu mimi mwenyewe jinsi nilivyo. “Kutana na wewe mwenyewe.” Ni wakati wa wewe mwenyewe kuwa, mshtaki, mshtakiwa, hakimu na mtetezi wa maisha yako.

Kuna Cartoon moja ya uswahili, inayomwonesha mzamiaji mmoja wa Bongo alipodaiwa kitambulisho na Polisi kiasi cha kukasirikiana kwa vile ndugu huyo hakuwa na kitambulisho chochote, wala kadi ya kupigia kura. Polisi alipozidi kudai kitambulisho, yule mzamiaji akaupangusa uso wake kwa mkono wa kushoto na kwa kidogo cha mkono wa kuume akawa anauonesha uso wake na kusema: “Hivi Bwana wewe Polisi unadhani sura yangu hii ni feki?”

Ni kweli kwamba, sura ya mtu inamdhihirisha mtu. Yawezekana hali na matendo yetu ni feki na hivi humsaliti mtu mwenyewe. Hiki ni kipindi cha kujijua, kujipembua endapo sura yetu ya ukristu, ya utawa, ya upadre ni halisi au feki. Baada ya kujijua unakuwa huru, mkweli ndani na nje mbele yako, mbele ya Mungu na mbele ya wenzako. Ni kama vile kuwa mkuu na kiongozi au raisi wa wewe mwenyewe. Mara nyingi kabla ya mmoja hajachaguliwa kuwa kiongozi kuna wakati anapohojiwa maswali na watafiti hasa waandishi wa habari juu ya kufaa kwake, mategemeo yake na vipeo vyake, na mambo atakayoyatekeleza. Inakuwa pia ni fursa ya kueleza sera zake za uongozi zitakavyokuwa.

Mwandishi wa habari naye budi awe amebobea katika uwanja wa siasa. Katika nafasi kama hizo ndipo wasikilizaji wanaweza kujua kama wanaye kiongozi bora au bora kiongozi atakayetuongoza kwenye nchi ya ahadi, yaani amani, maendeleo na umoja. Leo tutamshuhudia Yesu anavyowekwa kiti moto na shetani mara baada ya kuapishwa, yaani kubatizwa. Kwa kumfuatilia mahojiano hayo ya Yesu na shetani tutaweza hata nasi kupata majibu yatakayotusaidia kujielewa na kumjibu mwandishi wa habari malimwengu, aliyetuweka katika kitimoto cha dunia hii.

Yesu aliyefika duniani, baada ya kubatizwa anaenda Jangwani kufunga siku arobaini, huko anafikiwa na mtafiti aliyebobea na "kumuintaviu". Maswali yote anayosahiliwa Yesu yanahusu jinsi ya kuingiza siasa ya Baba yake itawale mioyoni mwa watu, yaani kutotilia wasiwasi upendo wa Mungu; uaminifu kwa Mungu, yaani kuaminia na kusadiki Neno la Mungu.

Maswali hayo yote ndiyo yanayoitwa vishawishi vya Yesu inayohusu maisha yake. Budi ielewe pia kwamba kabla ya kumhoji Yesu, mtafiti huyu alianza kwanza kuwaweka sawa watu wawili kwenye somo la kwanza. Kikao hicho kiliishia kufedheheshwa kwa kuvuliwa nguo hadi wenyewe wakakiri moja kwa moja kuwa “tupo uchi”. Sababu za kuingia fedheha hiyo ni kwamba aliyekuwa anawahoji alikuwa mwerevu kuwazidi “Basi nyoka alikuwa mwerevu kupita wanyama wote” Aidha, mtindo wa swali ulikuwa wa kukutia mashaka juu yako mwenyewe kama unajijua kweli au la.

Swali daima lilianza hivi: “Ati, Je ni kweli, Hivi ndivyo alivyosema Mungu msile matunda yua miti yote ya bustani?” Ujumbe mkuu ni kwamba, binadamu ametoka udongoni, ila amepata uhai kwa pumzi ya Mungu, kwa hiyo swali la msingi kwa binadamu ni hili: “Mtu ni nini” (Zab 8). Mtafiti anatumia mwanya huu wa kuijitambua binadamu anatoka wapi, anafika na swali dodoso na kumsahihisha mwanamke. “Mtakuwa kama Mungu.” Kwa hiyo kishawishi kikubwa sasa ni kutaka kuwa kama Mungu kwa sababu kufanana naye tu hakutoshi.

Hapa ndipo panapozaliwa homa ya msingi ya kutokukubali mipaka ya ukiumbe, kutokukubali kuwa sisi ni udongo na vumbi tu, huo ndiyo uhalisia wetu. Kutokujipokea uhalisia wake ndiko kunakomsababishia mtu kupata vishawishi vingine vingi, kutamani kwingi, kutaka kufanya miujiza, kuwa na ndoto za ajabu ajabu katika maisha. Hivi ni vishawishi vya msingi, ambavyo vipo kwa maisha yote na vipo ndani ya kila binadamu.

Utafiti aliofanya shetani kwa wazazi wetu wa kwanza ulihusu uchaguzi wakiwa ndani ya bustani ya miti, kulikokuwa na “mti wa uzima na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.” Ubaya unaozaliwa toka ndani ya moyo wa binadamu, anayeng’ang’ana kufuata maamuzi kadiri ya vigezo vyake, badala ya kufuata maamuzi na vigezo vya Mungu. Ubaya unaotokana na kukataa kujiingiza katika mradi wa kukua kiutu na kupima mambo vizuri kati ya wema na ubaya ukimtegemea Mungu. Kumbe mbele ya wema na ubaya mtu huwezi kujitegemea katika uchaguzi. Kufanya hivyo ni kujidai kuwa ni Mungu.

Katika Somo la Pili Paulo anamlinganisha Adamu na Kristu na matokeo ya mahojiano (vishawishi) na shetani. Kushindwa mahojiano kuliwatenganisha na Mungu na kutusababishia kifo kwa binadamu wote. Badala yake utii kamili wa Kristu umetuletea neema zote na uzima. Yesu ameziba tena mpasuko ule uliokuwa kati ya mtu na Mungu, na kufukia kabisa shimo lile lililotutenganisha na Mungu. Yesu anahojiwa na mtafiti yuleyule aliyewahoji Adamu na Eva. Mtindo wa kuhojiwa karibu unafanana, yaani anahojiwa juu ya uhalali wake wa kuwa mwana wa Mungu, ingawaje aliisha tamkiwa waziwazi wakati alipobatizwa kwamba “Wewe ni Mwanangu mpenzi niliyependezwa naye.”

Mahojiano yote yanaelekezwa kwenye uwepo wake, kadiri ya vigezo rahisi vya kibinadamu, yaani vinavyohusu mafanikio ya kibinadamu, kama vile ukuu au mamlaka, kujionesha, kujidhani au kujifikiria. Mtafiti huyu hakujua kwamba Yesu alichagua kigezo kingine kabisa, kile cha uaminifu katika kutekeleza mpango wa Mungu. Kwa vyovyote Yesu anataka kushikamana na hali yetu ya kibinadamu, hali ambayo alama zake ni ufukara na mateso, akichagua kwa ushujaa wote kuwa mtumishi wa wote. Aidha, kwenda kwake kuishi jangwani siku arobani, kwamaanisha kuishi maisha ya hapa duniani na kujaribiwa maisha yake yote. Hivi kila siku ya maisha, binadamu yuko kwenye kuhojiwa na shetani.

Kishawishi cha kwanza: “Ukiwa ndiwe mwana wa Mungu amuru mawe haya yawe mkate”. Shetani anaanza na swali linalohusu kula. Kwamba pale mtu akiwa na uhakika wa kula, hapo kila kitu ni salama. Hapa vinaingia vishawishi vyote vya binadamu vinavyohusu uchumi, mtazamo wake juu ya vitu, juu ya maisha kijumla, jinsi ya kujihami kiuchumi, kuhangaikia maisha zaidi kuliko ufalme wa Mungu na haki yake. Yesu anajibu: “Mtu haishi kwa mkate tu ila kwa kila neno litokalo mdomoni mwa Mungu.”

Huo ni mwaliko kwetu wa kutafuta katika Neno maelekezo ya jinsi ya kutatua matatizo yanayomsonga binadamu. Mkate ni mtamu lakini hauzidi utamu wa neno la Mungu chakula ni uhai, lakini uhai zaidi unatoka kwenye mdomo wa Mungu aliyetupumulia pumzi ya uzima. Tamko hilo la Yesu ndilo linaloamsha imani na linaipa maana maisha yetu, siyo tu kwa mtu binafsi bali kwa jumuia nzima ya kanisa pamoja na masakramenti na matendo yote ya imani (wongofu, kugawana, usafi wa maisha…), hizi ndizo thamani za kuziishi wakati huu wa kwaresima

Kishawishi cha pili: “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini, mwombe Mungu mwujiza”. Hii ni alama ya juu kabisa ya imani, yaani kujirusha chini toka mnarani. Huko ni sawa na kumpiga Mungu rushwa, yaani kulaghai ukuu wa Mungu katika kutekeleza mpango wako wa kibinadamu. Mungu hatupatii uwezo wake ili tuoneshe ubabe wetu, bali anatudai kuwajibika kwetu na kuongoka kwetu.

Ni kishawishi kikubwa cha kukosa saburi au uvumilifu, kishawishi cha kutaka kupata au kuona mapato ya pekee, makubwa, sasa hivi, ni kishawishi cha kutaka kutatua matatizo bila ya kujidhatiti, na kuubadili ulimwengu bila kutoka jasho. Kumbe maisha yanadai saburi sadaka, imani. “Subira yavuta heri.”

Kishawishi cha tatu: “Ukianguka kunisujudia” kishawishi hiki chahusu mahusiano na wengine (njaa na kiu ya madaraka, kushabikia mno nguvu), ni ndoto ya kutaka kutatua matatizo yetu kwa njia ya kufifisha maadili na kuthamanisha zaidi miradi na mambo ya ukuu wa ulimwengu huu. Hiki ni kishawishi cha ukuu kama ndiyo thamani ya kwanza ya maisha. Vishawishi hivi alivyopewa Yesu, karibu ni vile vile walivyojaribiwa Waisraeli jangwani, kabla ya kuingia nchi ya ahadi. Nasi pia tutafakari vyema tukiwa bado tunasafiri katika bonde hili la ulimwengu, tukielekea mbinguni kwenye nchi ya ahadi.

Tunahojiwa daima na mtafiti shetani. Silaha aliyotumia Yesu ni ile ya Neno la Mungu, ya imani na ukweli. Yesu akisukumwa na Roho jangwani anashinda vishawishi na kutoka mshindi. Yesu anatukumbusha kwamba imani yataka kujitoa kabisa na kumwaminia Mungu anayetujia na tumpokee kwa unyenyekevu. Tumwombe tukisali “Uturehemu Ee Bwana, kwa kuwa tumetenda dhambi” (Zab 50).

Tukitumie vyema kipindi hiki cha Kwaresima kilicho mwafaka kwetu wa kukutana na wewe wenyewe na kukutana na Mungu atakayekuwezesha kukutana na wengine katika haki na upendo wa Mungu.
P. Alcuin Nyirenda, OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.