2014-03-08 15:50:36

Askofu mkuu Obbo wa Jimbo kuu la Tororo Uganda asimikwa rasmi


Askofu mkuu Emmanuel Obbo, hivi karibuni alisimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tororo, Uganda, katika Ibada iliyohudhuriwa na Askofu mkuu Michael August Blume, Balozi wa Vatican nchini Uganda, Maaskofu, watawa na waamini walei. Rais Yower Kaguta Museveni alikuwa ndiye mgeni rasmi katika sherehe hizi. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mashahidi wa Uganda, Nyangole, Jimbo kuu la Toror, Uganda.

Askofu mkuu Obbo katika mahubiri yake kwanza kabisa alimshukuru Mwenyezi Mungu, aliyemwita na kumchagua kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tororo, Uganda na kwamba, kila Kristo anaalikwa kwaza kabisa kuchuchumilia utakatifu wa maisha na baadaye miito mingine ndani ya Kanisa. Hakuna sababu ya kuogopa kwani Mwenyezi Mungu anayemwita mja wake atamkirimia neema na baraka anazohitaji katika kuwatakatifuza watu wa Mungu, kuwafundisha na kuwaongoza kwa kufuata mfano wa Kristo mchungaji mwema.

Askofu mkuu Obbo anasema Wakristo wanaalikwa kumpenda Mungu na jirani kwa kuwatumikia wananchi kwa moyo mkuu, weledi, juhudi na maarifa. Katika kipindi hiki, Mama Kanisa anaendelea kurudia ujumbe wa Kristo wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mwenyezi Mungu, kwa kujenga na kuimarisha urafiki na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani.

Upendo unaobubujika kutoka katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu hauna budi kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini ndani ya familia na Jamii katika ujumla wake. Chuki, uhasama na magomvi ndani ya familia na Jamii ni mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Rais Yoweri kaguta Museveni wa Uganda, katika nasaha zake wakati wa kumsimika Askofu mkuu Emmanuel Obbo, amelishauri Kanisa kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Serikali katika utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kilimo na maendeleo endelevu kwa wananchi wa Uganda. Ameliomba Kanisa kusaidia mchakato wa maboresho katika shughuli za uchumi na maendeleo, ili kuwajengea wananchi uchumu utakaolisaidia hata Kanisa kuweza kujitegemea.

Rais Museveni anasema, haogopi nchi za Magharibi kusitisha misaada yao kwa Uganda kwa sababu ya kupitisha muswada wa sheria unaokataza vitendo vya kishoga nchini Uganda, bali anapania kuhakikisha kwamba, wananchi wa Uganda wanasimama kidete ili kujiletea maendeleo yao wenyewe badala ya kusburi misaada inayodhalilisha utu na heshima yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.