Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima
Mpendwa msikilizaji, leo tunatafakari masomo Dominika ya kwanza ya Kwaresima, kipindi
cha mfungo mtakatifu. Kipindi ambacho cha kusali, kufunga na kupigana na mwovu shetani.
Kwa sala tunamwomba
Mungu ujasiri wa kubadili maisha yetu ili tuambatane na Injili. Kwa kupigana na mwovu
mkristu ataka kutawala hisia na vionjo vinavyokuza ubinafsi. Kwa kufunga mkristu hujikusanyia
siraha, kwa ajili ya mapambano na hivi katika kufunga huweza kujitoa kuacha vitu ambavyo
anaviona ni vya maana na hivi kwa kwa ajili ya kuwasaidia maskini. Kwa kuwasaidia
wengine mkristu hujichagulia umaskini wa roho na hapa ndipo kuna kufunga kwa uhakika.
Neno la Mungu Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima latualika kutafakari juu
ya MAJARIBU (vishawishi).
Katika somo la kwanza toka kitabu cha Mwanzo tunapata
simulizi juu ya Adamu na Eva wanaoishi katika bustani iliyojaa matunda na uzuri wa
kila aina. Katikati ya bustani hii kuna mti maalum wa matunda ambao ndugu hawa hawakuruhusiwa
kuugusa, kwa maana ulitengwa kwa ajili ya Mungu tu. Mti huu kwa hakika si rahisi kujua
ni mti wa matunda yapi, lakini kwa hakika mwandishi ataka kuwasilisha mbele yetu “mti
wa mema na mabaya”. Ni alama inayowakilisha zuio au mipaka ya utendaji wa mwanadamu.
Ni kwa jinsi hii tunatambua kuwa Mungu alimwumba mtu akiwa huru lakini ndani
ya mipaka ya uwezo wake, yaani juu ya wema na ubaya hakuwa na nguvu ya kudai au kuamua!
Ni Mungu pekee mwenye uwezo wa kupambanua wema na ubaya. Ni katika mantiki hii basi
Mwanadamu alipotaka kwa kiburi chake kutambua wema na ubaya, akaangukia katika shimo
la uharibifu. Hakuweza kuwa sawa na Mungu kama alivyofikiria bali ndo akawa amepoteza
hata kile alichokuwa nacho!, akawa ameangukia katika kutawaliwa na vionjo na hisia
zake na hivi hata kuweza kuchanganya mambo yaani kibaya anakiona chema na chema anakiona
kibaya! Hali hii ipo leo katikati yetu au hakuna)? Tutafakari maisha yetu ya sasa!
Mpendwa
msikilizaji tumeona sura ya mwanadamu ilivyokuwa na ilivyogeuka baada ya majaribu
na kuwa saliti, inatupeleka kuona sura ya Bwana wa Agano jipya ilivyokuwa kabla ya
vishawishi na baada ya vishawishi na hasa alivyovumilia na kushinda na hivi akatimiza
mapenzi ya Mungu, kwa ajili ya wokovu wetu. Yafaa sasa kuona sura ya nyoka, tukijiuliza
hivi mwandishi ataka kusema nini? Nyoka awakilisha kishawishi na kishawishi ni kutengana
na Mungu. Ni kujikomaza katika ubinafsi na kumweka Muumba wangu pembeni kana kwamba
naweza kuongoza maisha yangu mwenyewe!
Kishawishi huingia polepole na kwa
siri katika moyo wa mtu kama nyoka alivyojipenyeza katika maisha ya Adamu na Eva.
Uzuri wa mti wa matunda ulianza kujipenyeza katika hisia zao baada ya kushtuliwa na
nyoka! Kwa hakika haikuwa rahisi kuchomoka kwa sababu tayari kiburi na majigambo yalikuwa
yamekwishaingia moyoni mwao.
Mpendwa msikilizaji, kwa kumwacha Muumba mtu hujishusha
toka hadhi yake ya mwanzo yaani hali ya kuwa huru na huanza kujisikia na kujiona uchi,
na kwa namna hii hurudia hali ya kuwa kama mnyama ambaye hana cha kujisetiri! Mtu
kwa kumwacha Mungu huingia katika laana na hivi chanzo cha vita, magomvi, wivu, ufisadi
na mambo kama hayo. Kwa hakika laana hii imejifungamanisha katika dhambi na si kwamba
Mungu huacha kumpenda mwanadamu. Ndiyo kusema kwa kutenda dhambi mtu hujiadhibu mwenyewe,
huharibu ndoa yake, huharibu masomo yake, kazi yake na urafiki nk.
Mpendwa
msikilizaji Neno la Bwana halituambii kilichotokea tu mwanzoni bali kile kinachotokea
hivi leo katika maisha yetu ya kila siku. Kwa kuweka pembeni Neno la Mungu maana yake
tunatangaza kupotea toka njia mapendo na ya uhuru na kuingia katika upotevu na uharibifu
wa maisha yetu.
Mpendwa mwana wa Mungu, Mt Paulo anapowaandikia Warumi anaonesha
waziwazi tofauti kati ya Adamu na Kristu Masiha. Adamu kwa kukosa utii kwa Mungu anapoteza
uhuru wake na kuzama katika taabu na badala yake Kristu anamtii Baba yake na kwa njia
hiyo ya utii mkamilifu anakuwa mfalme wa maisha na mwokozi wa Adamu na watu wote kwa
ujumla. Sisi tunataka nini? maisha au taabu! Kama ni maisha basi utii ndiyo njia pekee
katika kwaresima hii kuelekea uhuru kamili kama alivyokusudia Mwenyezi Mungu tangu
mwanzo kabla ya anguko.
Katika somo la Injili tunapata kumwona Bwana ambaye
anabaki mwaminifu kwa Baba yake, mbele ya majaribu, mbele ya shetani ambaye alitaka
kumtoa katika msimamo wake wa kitume. Majaribu kwa Bwana yalikuwa daima mbele yake
katika kipindi chote cha uchungaji. Kumbuka pale mwishoni mwa safari yake aliposema
“Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Ndiyo kusema majaribu tunayoyasikia katika
Dominika hii ni ufupisho wa majaribu yote ambayo Bwana ameyapitia na akashinda!
Mwinjili
Matayo ataka kutukumbusha kwa njia ya majaribu haya matatu, yale majaribu kwa Waisraeli
huko jangwani tokea Misri. Jaribu I lahusu mkate na katika hili Bwana anapelekwa jangwani
kama Waisraeli na anakaa huko siku 40 kama Waisraeli walivyokaa miaka 40 jangwani.
Bwana anakemea jaribu hilo akisema mtu hataishi kwa mkate bali kwa kila Neno litokalo
katika kinywa cha Mungu. Anasisitiza mambo ya kiroho kama njia ya wokovu na ataka
kusema kwamba mali haitoshi bali muhimu amani na upendo katika maisha yetu. Fikiria
mtu mmoja ana magari na mijumba ya kutosha lakini nyumbani ugomvi kila siku, kuna
furaha katika mali ile? Tafakari!
Mpendwa, jaribu II lahusu hakikisho la kuwa
kweli Mwana wa Mungu. Katika hili kumbukeni Waisraeli walipokuwa jangwani walimjaribu
Bwana akawape maji toka katika mwamba! Na kwa namna haiyo walitaka kuhakikisha uwepo
wa Mungu na upendo wake kwao! Kinyume cha fikra hizi Bwana anakataa kuomba ishara,
hahitaji kuhakikisha upendo wa Mungu kwake maana upo na inaeleweka. Katika siku zetu
hizi kuna kishawishi cha kutaka kuhakiki upendo wa Mungu kwetu, mfano mmoja anasema
“Mungu kama wanipenda naomba nipate kazi!! Na pengine asipopata anaanza malalamiko.
Hatupaswi kuomba namna hii bali kwa matumaini na hivi mapenzi yake yatimizwe.
Mpendwa
jaribu la III lahusu madaraka na miliki za ulimwengu. Katika hili Waisraeli walipokuwa
jangwani, walionekana kwa wakati fulani kumchoka Mungu wao na hivi wakaanza kujitengenezea
visanamu na kuviabudu. Bwana akitambua hatari hii anakataa kabisa kuabudu vijisanamu
vya kujitengenezea, anakataa kabisa kuiabudu siasa, fedha, mafanikio na nguvu za kivita
bali anabaki mwaminifu kwa Baba yake. Kwa wakati wake walitarajia Masiha mwenye nguvu
lakini Bwana anajitokeza kinyume chake na kuonesha unyenyekevu upeo na hasa akitaka
kuwashirikisha uhuru walio maskini na wenye dhambi.
Mpendwa msikilizaji, Bwana
anashinda mambo haya yote na hii ndiyo kwaresima kwake, ndiyo kwaresima yetu tunapoelekea
katika heri ya milele. Tunapaswa kubaini daima mitego ya mwovu na kuweza kupambana
nayo kwa ujasiri tukitumia siraha ndilo Neno la Mungu. Mpendwa ninakutakia furaha
na matumaini katika maisha yako daima ukimtanguliza Mungu na kwa namna hiyo kuijua
hekima ya kweli ijengayo nguvu ya kushinda majaribu dhidi yako. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.