Mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa duniani unaweza kupata mafanikio makubwa
kwa kuwajengea wanawake uwezo kwa njia ya elimu makini ili waweze kushiriki kikamilifu
katika uzalishaji kwenye sekta ya kilimo.
Shirika la Mpango wa Chakula la
Umoja wa Mataifa katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa tarehe
8 Machi, 2014 linaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwajengea uwezo wanawake ili kupambana
kikamilifu na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula pamoja na utapiamlo unaoendelea
kusababisha maafa makubwa kwa watoto sehemu mbali mbali za dunia.
Kauli mbiu
ya Maadhimisho ya Mwaka huu inajikita zaidi katika usawa katika Jamii, jambo ambalo
linapaswa kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali, ili kuboresha ushiriki wa wanawake
katika mchakato wa maendeleo endelevu. Wanawake wanaojishughulisha na kilimo wawezeshwe
kuzalisha mazao ya chakula na biashara, ili kuwa na uhakika wa chakula pamoja na kujijengea
uwezo wa kiuchumi. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO linasema
kwamba, ikiwa kama wanawake watawezeshwa kikamilifu katika uzalishaji wanaweza kusaidia
kupunguza kiasi cha watu millioni mia moja wanaoteseka kutokana na baa la njaa duniani.
Wanawake
wamepewe haki ya kumiliki ardhi, wapate mikopo na pembejeo za kilimo, tayari kushiriki
kikamilifu katika mchakato wa uzalishaji katika sekta ya kilimo. Wanawake wakiwezeshwa
katika elimu na kilimo, baa la njaa na utapiamlo vitapewa kisogo duniani. Siku ya
Wanawake Duniani ilianza kuadhimishwa mwaka 1975 na Umoja wa Mataifa.