Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kilichokuwepo nchini Sierra Leone, kwa
kipindi cha miaka kumi na mitano, kimehitimisha kazi yake na kufunga vilago, dalili
kwamba, amani na utulivu vimerejea tena nchini humo. Vita iliyotokea nchini Sierra
Leone kati ya Mwaka 1991 hadi kufikia mwaka 2002 vilisababisha vifo vya watu 50, 000
na nusu ya wananchi wa Sierra Leone walilazimika kuyakimbia makazi yao.
Katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Kimoon akizungumza na waandishi wa habari mjini
Freetown amekiri kwamba, Sierra Leone ni kati ya nchi ambazo zimefanikiwa kurejesha
amani na utulivu na kwamba, kwa sasa Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa linaweza
kuondoka na kuwaacha wananchi wakiwa katika hali ya amani na usalama.
Changamoto
kubwa iliyoko mbele ya Sierra Leone ni kuhakikisha kwamba, inatumia vyema rasilimali
yake kwa ajili ya mchakato wa mapambano dhidi ya baa la ujinga, umaskini na maradhi
yanayoendelea bado kusababisha majanga makubwa kwa wananchi wengi wa Sierra Leone.
Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, rushwa na makundi ya uhalifu
ni kati ya mambo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na Serikali ya Sierra Leone, ili
kweli amani na utulivu vilivyopatikana kwa kumwaga damu ya wananchi wasiokuwa na hatia
iweze kudumu na kuwa ni kikolezo cha ustawi na maendeleo ya wananchi wa Sierra Leone.