2014-03-07 11:53:24

Kwaresima kiwe ni kipindi cha kuombea amani na utulivu duniani kote!


Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; ni fursa ya kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo; ni wakati uliokubalika wa kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea haki, amani, upendo na mshikamano duniani kote. Ni changamoto inayotolewa na Askofu Santo Marcianò wa Jimbo la Kijeshi nchini Italia katika ujumbe wake wa kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2014.

Kwaresima ni kipindi kinachomwezesha mwamini kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kusherehekea Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Ni mwaliko kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa waamini kuingia katika undani wa maisha yao na kuanza hija ya toba na wongofu wa ndani, ili kujenga msingi wa upendo na mshikamano wwa kidugu. Toba na wogofu wa ndani ni mwaliko wa kuitafuta njia mpya ya maisha inayooneshwa na Mwenyezi Mungu kwa waja wake, baada ya kuchunguza dhamiri.

Kwaresima ni kipindi cha kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo na udugu kati ya watu, lakini zaidi kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kwa njia ya matendo ya huruma yanayobubujika katika undani wa moyo wa mwanadamu. Matendo haya yafanyike katika usiri na wala hakuna haja ya "kupiga mayowe" wala kujikuza kwa kuwasaidia watu wenye shida kwani huu ni wajibu msingi katika maisha ya Kikristo. Matendo ya huruma yauguse undani wa maisha ya mwamini kabla ya hata kunyoosha mkono ili kutoa sadaka kwa maskini.

Kipindi cha Kwaresima iwe ni fursa kwa waamini kusali, kufunga na kumwabudu Yesu Kristo kwani waamini wameijua neema ya Kristo jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yao, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba, wao wapate kuwa matajiri kwa umaskini wake, kama anavyofafanua Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka huu.

Askofu Santo Marcianò anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukitumia kipindi cha Kwaresima kwa ajili ya kusali na kuabudu mbele ya Ekaristi Takatifu, ili kuombea amani na utulivu sehemu mbali mbali za dunia. Inasikitisha kuona na kusikia kwamba, vita na mahangaiko ya watu si tena habari inayowashtua watu, kwani wamezoea na wala hakuna jambo jipya hapa. Hii ndiyo hatari liyopo anasema Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, watu wasipende kuzoea vita na mahangaiko ya watu.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini katika ujumbe wake wa Kwaresima kwamba, kuna aina mbali mbali za umaskini katika maisha ya mwanadamu: kuna umaskini wa kipato usikuwa na matumaini wala mshikamano wa kidugu; kuna umaskini mkubwa wa kimaadili unaoendelea kuwatumbukiza watu katika majanga mbali mbali ya maisha na mwishoni, kuna umaskini wa maisha ya kiroho, unaotaka kumng'oa Mwenyezi Mungu kutoka katika maisha ya binadamu. Ukosefu wa amani na utulivu ni kati ya maafa makubwa yanayomkabili mwanadamu wa leo, kwani amani ni jina jipya la maendeleo.

Mama Kanisa katika kipindi hiki cha Kwaresima anawahamasisha watoto wake kujiandaa katika adhimisho la Fumbo la Pasaka kwa njia ya Sala, toba na wongofu wa ndani; kwa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu kama sehemu ya imani tendaji pamoja na kufunga kama njia ya kudhibiti vilema na mapungufu ya kibinadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.