2014-03-06 12:19:18

Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: TAMKO


Tamko “matumaini na furaha ya watanzania kwa ujio wa Rasimu ya katiba iliyosheheni utu na misingi ya kujali maslahi ya wote”

Mkutano wa kitaifa wa wajumbe wa kamati za majimbo za Haki na Amani za Kanisa Katoliki Tanzania pamoja na Wanataaluma Wakristo wa Tanzania (CPT), walikutana kwenye Kituo cha kiroho cha Mbagala, Jijini Dar es Salaam, tarehe 5 – 6 Februari, 2014.

Wakitafakari juu ya mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wajibu wa Kanisa Katoliki katika Utume wake wa Kinabii wa kulinda na kujenga haki na amani nchini mwetu, walimshukuru Mungu kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya uwenyekiti wa Jaji Joseph Sinde Warioba, kufanikiwa kuwasilisha rasmi Rasimu Na. 2 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 30 Desemba, 2013 na kuashiria mwanzo wa hatua ifuatayo ya kuunda Bunge Maalumu la Katiba.

Baada ya kuipitia Rasimu hiyo kwa kuongozwa na uchambuzi makini uliowasilishwa na Sekretarieti ya Tume ya Haki na Amani wajumbe wameridhia kwamba :

    Kwa hakika Rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni ya watu na sio ya wanasiasa au vyama vya siasa wala asasi za kidini. Kwa sababu hiyo tunatoa mwaliko kwa kila raia wa Tanzania kufurahia ushiriki wake kufikia Rasimu Na. 2 yenye mambo bora yatakayokuwa nguzo ya umoja wa nchi yetu katika Katiba Mpya.


    Maadili yaliyomo katika Rasimu Na. 2 ni muhimu kabisa kwa taifa letu.
    Wananchi na viongozi wote sharti wajali maslahi kwa wote na wasimamie haki na wajibu wa kila mtu.


    Madhumuni ya msingi ya Katiba ni ustawi wa kila Mtanzania, haki za kiuchumi, usalama, kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa na haki kwa wote pasipo ubaguzi kwa madhumuni ya kulinda amani.


    Katiba yetu lazima isiruhusu wachache wenye nguvu za kisiasa, kiuchumi na kiutawala kutumia vibaya uwezo wao na kusababisha utengano kitabaka katika jamii huku wakijinufaisha kwa kutumia rasilimali za nchi zilizo za wote. Pawepo na udhibiti thabiti wa mienendo ya namna hiyo na uwajibishaji makini kwa wabadhilifu wa mali ya umma.


    Katiba ni chombo hai kwa ajili ya kuhudumia jamii na sio jamii kuhudumia Katiba. Kwa sababu hiyo yatupasa kuthubutu kubuni njia mbadala ili kukuza kipato cha raia wa kawaida na kuboresha huduma za jamii kwa kuwa na mipango endelevu ya kiuchumi.


    Pendekezo la Muundo wa Muungano wa serikali tatu sio jambo kuu kuliko mengine yote katika Rasimu hii. Muundo wa serikali mbili haukutatua matatizo msingi bali ulilimbikiza kero zilizosababisha Zanzibar kujiundia katiba yake mpya ya mwaka 2010 bila kushauriana na Tanzania Bara (Tanganyika). Pendekezo la serikali tatu lililowekewa mazingira tekelezi yakitoa mwanya wa kuboresha muundo huo kwa njia wazi, shirikishi na za kidemokrasi lina tija kubwa ya kuturudishia hali ya kuwa wamoja.


    Mihimili mikuu mitatu; Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Bunge la Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Jamhuri ya Muungano ni taasisi mpya kabisa kwa mujibu wa Rasimu Na. 2 zitakazoongoza, kuratibu na kuwajibisha kila kiungo cha Jamhuri ya Muungano zikiwemo serikali za Nchi Washirika.


    Haki ya mtu ya kuishi lazima ilindwe na Katiba kuanzia pale mimba ya binadamu inapo tungwa katika mama na katika hatua zake zote za kumhudumia mama mjamzito.


    Kumtambua Mungu na kumtaja katika Katiba yetu kunamaanisha kukiri kwetu Uwepo Wake aliye Muumba wetu na vitu vyote ambavyo mwanadamu anavitegemea kwa uhai wake. Mungu anakuwa rejelea yetu katika kuheshimiana kiutu. Ni chimbuko la utu wa binadamu. Kwa kuwa katika Wimbo wetu wa Taifa tunamwomba Mungu baraka zake ili tufanikiwe na tuishi kwa amani, ni hekima na busara kumkiri katika Sheria Mama – Katiba.


Tunapoelekea kwenye Bunge Maalum la Katiba tunataka mambo yafuatayo ya msingi kabisa yatambuliwe na kufahamika kwa wote:

    Watanganyika na Wazanzibar tuwe na nia madhubuti ya kuwa wamoja.


    Haki za binadamu za kisiasa, kiuchumi na kijamii zipatikane na kufurahiwa na wote. Umasikini na ufinyu wa bajeti ya serikali ni visingizio tu vya mamlaka kutokutoa haki kwa wote.


    Yatupasa kukiri mapungufu yetu katika serikali zetu na itikadi za kisiasa kusudi kwa moyo wa unyenyekevu na mkunjufu tuanze safari mpya katika mwanga mpya wa maridhiano. Pamoja na kukiri kasoro za wakati uliopita tujivunie maendeleo tuliyofanya katika kila nyanja za maisha wakati tukiboresha mifumo na miundo ya utawala.


    Ulimwenguni hakuna katiba yoyote kamilifu. Yatupasa tuanze na Rasimu iliyopendekezwa na tuendelee kuiboresha pale itakapobidi.


    Tunawasihi wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuweka kando itikadi za vyama vyao kama walivyofanya Wanatume wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika kuandaa Rasimu Na. 2. Bunge Maalum la Katiba lilenge kufanikisha mchakato mwema wa Katiba Mpya itakayoandaa njia na mifumo mipya ambayo kwayo tutahakikishiwa kuwepo kwa taratibu wajibishi na wajibikaji ili kuendeleza ustawi wa jamii na muundo wa Muungano utakaokuwa wazi na tayari wakati wote kuboreshwa kwa manufaa ya Watanzania wote.


    Katiba Mpya ya Tanzania itakuwa na fursa ya “FURAHA MPYA SHIRIKISHI” kwa Watanzania wengi. Rasimu na. 2 ni hatua njema katika tukio muhimu la kihistoria nchini tanzania. Tunatarajia bunge maalum lisimkane Mungu na lisikashifu mapendekezo ya serikali tatu.


Tunawaalika wananchi wote wa Tanzania kwa dhamira moja, kuliombea na kulisaidia Bunge Maalum la Katiba, liweze kufanya kazi yake kwa ustadi na kujali maslahi ya Taifa na wananchi wote wa Tanzania.



Askofu Mkuu Paulo Ruzoka
MWENYEKITI
Tume ya Haki na Amani - TEC








All the contents on this site are copyrighted ©.