Balozi wa Vatican aanza utume wake nchini Pwani ya Pembe
Hivi karibuni Askofu mkuu Joseph Spiteri, Balozi Mpya wa Vatican nchini Pwani ya Pembe
aliwasili nchini humo na kupokelewa na viongozi wa Kanisa na Serikali kwenye Uwanja
wa ndege wa Kimataifa mjini Abijan. Askofu mkuu Spiter baadaye alikutana na kuzungumza
na Bwana Charles Koffi Diby, Waziri wa mambo ya nchi za nje, nchini Pwani ya Pembe,
ambaye alimpatia nakala ya hati zake za utambulisho.
Tarehe 18 Desemba 2013,
Askofu mkuu Joseph Spiter aliwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais Alassane
Ouattara katika hafla ya kitaifa iliyokuwa imeandaliwa kwa heshima yake. Viongozi
hawa wawili katika mazungumzo yao, wameridhika na uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican
na Pwani ya Pembe; kati ya Kanisa na Serikali katika mchakato wa haki, amani na upatanisho
bila kusahau mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa Katoliki katika sekta ya elimu, afya
na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Kanisa linaendelea kujipambanua
katika huduma zake kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Rais Alassane Ouattara amekumbusha kwa shukrani ziara ya kiserikali
aliyoifanya mjini Vatican kunako 16 Novemba 2012 kwa kukutana na kuzungumza na Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI.
Askofu mkuu Joseph Spiteri amewasilisha salam
na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, anapenda kutekeleza
utume wake miongoni mwa Familia ya Mungu nchini Pwani ya Pembe kama mhudumu wa Injili
anayependa kujenga na kudumisha udugu na mshikamano kati ya watu, ili kujenga na kudumisha
utamaduni wa amani, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.
Ilikuwa ni tarehe
14 Januari 2014, Askofu mkuu Joseph Spiteri alipowasilisha hati zake za utambulisho
kwa Askofu Touabli Youlo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe kwa kutiwa
mkwaju na aliyekuwa Askofu mkuu Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ambaye hivi
karibuni alisimikwa kuwa Kardinali. hafla hii imefanyika katika Maadhimisho ya Fumbo
la Ekaristi Takatifu, wakati ambapo Baraza la Maaskofu Pwani ya Pembe lilikuwa linaadhimisha
mkutano wake wa 97.