Bado kuna watoto 50, 000 wanakabiliwa na utapiamlo na ukosefu wa huduma za afya nchini
Somalia
Baa la njaa lililoikumba Somalia kunako mwaka 2011 linaanza kutoweka na kuna maendeleo
pia katika masuala ya kisiasa ingawa bado kuna vitisho vya mashambulizi ya kigaidi.
Licha ya Somalia kuanza kuonesha cheche za maendeleo, lakini Umoja wa Mataifa pamoja
na Serikali ya Somalia inawahimiza wafadhili mbali mbali kuendelea kuchangia katika
ustawi na maendeleo ya Somalia. Kuna zaidi ya watoto 50, 000 wanaokabiliwa na utapiamlo
wa kutisha pamoja ukosefu wa huduma msingi za afya.
Jumuiya ya Kimataifa kwa
sasa inaelekeza misaada yake Sudan ya Kusini, Syria na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya
Kati ambako watu kwa sasa wanakabiliana na maafa makubwa. Lakini Serikali ya Somalia
inasema, bado wanahitaji msaada kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kuokoa maisha
ya watoto wanaokabiliwa na utapiamlo wa kutisha pamoja na ukosefu wa huduma msingi
za afya.
Rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma pamoja na misaada inayotolewa
kwa wananchi wa Somalia ni kati ya mambo yanayokwamisha utoaji wa misaada inayopelekwa
nchini Somalia, kadiri ya taarifa ya Umoja wa Mataifa. Bado asilimia 60% ya watu wapatao
millioni 3.5 wako chini ya utawala wa Kikundi cha Kigaidi cha Al Shabab, Kusini mwa
Somalia. Umoja wa Mataifa unaohifia kwamba, ikiwa kama wananchi watashambuliwa wakati
huu wa kutayarisha mashamba, mavuno hapo mwakani yanaweza kuwa ni hafifu.