Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, kwa mara nyingine karibu katika Kipindi chetu
cha Kanisa la nyumbani, ambapo leo, tunaandaana kuanza safari yetu ndefu na muhimu
sana ya mfungo wa siku arobaini (mfungo wa Kwaresma), tutakayoianza siku ya Jumatano
ya majivu. Katika kipindi
hiki cha siku 40, mama Kanisa anatualika sisi sote kushughulikia kwa jitihada kubwa
zaidi uongofu wetu sisi wenyewe. Masomo matakatifu pamoja na tafakari nyingi, zitatuelekeza
kujitafiti katika roho ya ukweli wa ndani, tujifahamu tulivyo ili tujirekebishe pale
ambapo hatukwenda sana na tujiimarishe zaidi pale ambapo kwa neema ya Mungu tuliweza
kwenda sawa. Daima sote tunaalikwa kuongeza na kuimarisha maisha ya fadhila mbalimbali. Kwaresma
ni kipindi cha kujipatanisha kwanza na nafsi zetu. Kuna nyakati tumejitendea mambo
makubwa maovu sana, hata tukaanza kujichukia sisi wenyewe, tumejikatia matumaini,
tunajiona hatufai tena na tunahisi kuwa hatupendwi na wenzetu. Hatua ya kwanza ya
wongofu ni kujifahamu, pili ni kujikubali na tatu ni kuwa tayari kujisamehe na kujirekebisha.
Acha ya kale, anza upya, songa mbele. Kwaresma ni kipindi cha kumrudia Mungu kwa
mioyo yetu yote. Kwa kinywa cha Nabii Yoeli mwenyewe asema “...nirudieni mimi kwa
moyo wote, kwa kufunga, kulia na kuomboleza” Yoel 2:12. Katika roho ya ukweli wa ndani,
kila mmoja katika familia anajua ni namna gani amejiweka mbali na Mungu, na kwa kitendo
cha kuwa mbali na Mungu, wewe katika familia umekuwa ndio uchochoro wa shetani, anayeingia
katika familia ili kuivuruga. Bwana akuita kwa upole, asema nirudieni mimi kwa moyo
wote. Kwaresma ni kipindi cha kutoa sadaka sana, kusali sana kwa moyo wa toba ya
ndani na kufunga (Rej. Mt. 6:1-6, 16-18). Hii ni sehemu ya habari njema inayosomwa
siku ya Jumatano ya Majivu. Katika sehemu hii Bwana anatupatia nidhamu ya kutoa sadaka,
kusali na kufunga ili kweli tupate mafaa ya kiroho. Na sisi kama familia tunapenda
kwaresma hii tuwe na sadaka ya pamoja kama familia, tuwe na sala za pamoja zaidi na
tuuchukue mfungo huu kwa pamoja. Wataalamu wa mambo ya roho wanatuambia, kufunga
ni namna bora zaidi ya kufanya kitubio na kujipatia nguvu mpya ya roho. Kwa ujumla
wake katika kipindi hiki cha Kwaresma, sisi wana kanisa la nyumbani yaani familia,
tutatafakari sana juu ya tunu za toba na msamaha. Tutakiri kwamba, katika familia
zetu mara nyingi tumekoseana na kujeruhiana vibaya sana, kiasi kwamba tumeathiri vikali
ule UZURI wa maisha ya ndoa na familia. Kwa matendo yetu tumeifukuza haki, tumefukuza
upendo, tumefukuza amani na furaha ya familia. Dawa yetu ni mmoja tu – toba na msamaha,
tufanye toba ya kweli, tusameheane na tuwe tayari kujirekebisha kabisa. Familia
nyingi zimekonda na kunyauka vibaya, hazijui tena kicheko wala tabasamu, wala utani
kwa sababu wanashindwa kuombana msamaha wa kweli na kusameheana. Wengi wanapenda zaidi
maisha ya ubabe na umame ambayo hayajengi familia kamwe. Ugangwe, jeuri, kiburi na
roho mbaya vinaelekea kutawala katika familia zetu!! Vilio vimezidi katika Kanisa
la nyumbani. Nani anyamazishe? Ni MIMI NA WEWE. Baba Mtakatifu Fransisko anatufundisha,
maneno matatu yanayoifanya familia isonge mbele ni NAOMBA, SAMAHANI na ASANTE. Katika
Kwaresma hii tutalitafakari sana hilo lihusulo KUOMBA MSAMAHA, KUTUBU KWA MANENO NA
VITENDO, na KUFANYA JITIHADA YA KUJIREKEBISHA. Usijitese kwa kutokuwa tayari kutubu,
na usijiangamize kwa kutokuwa tayari kusamehe. Mume jipatanishe na mkeo, mke jipatanishe
na mumeo, wazazi jipatanisheni na watoto wenu, watoto, jipatanisheni na wazazi wenu.
Msamaha na mapatano mema VINAWEZEKANA. Bwana Mungu atuumbie mioyo safi na atengeneze
tena roho thabiti iliyotulia ndani mwetu. Tunawaweka mikononi mwa Mungu na tunawatakieni
nyote Kwaresma njema. Kutoka katika Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Pambo Martin
Mkorwe OSB.