Waziri mkuu Ponta wa Romania akutana na Papa Francisko mjini Varican
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 1 Machi 2014 amekutana na kuzungumza na
Waziri mkuu Victor Ponta wa Romania, ambaye baadaye alikutana na Kardinali Pietro
Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Dominique Mamberti,
Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.
Waziri
mkuu Ponta amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Patriaki Daniele wa Kanisa
la Kiorthodox. Kiini cha mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake
kilikuwa ni familia, elimu, uhuru wa kidini na umuhimu wa kusimama kidete kulinda
na kutetea tunu msingi za maisha ya kiutu na kiroho zinazojipambanua katika ushirikiano
kati ya Vatican na Romania mintarafu Jumuiya ya Kimataifa.
Viongozi hawa wamepongeza
mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa Katoliki nchini Romania kwa ajili ya ustawi na
maendeleo ya wananchi wa Romania. Wamegusia pia mambo yanayopewa kipaumbele cha kwanza
na Kanisa Katoliki nchini humo. Mwishoni, viongozi hawa wawili wamebadilishana mawazo
kuhusu hali ya kimataifa kwa kukazia umuhimu wa majadiliano ya kina ili kukomesha
vita na kinzani za kijamii zinazoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia.