Onesheni imani katika matendo kwa kuchangia Nchi Takatifu
Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki limepokea changamoto na wasi wasi
uliooneshwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, linawaalika
waamini wa Makanisa mahalia sehemu mbali mbali za dunia, kuonesha mshikamano wao wa
dhati kwa Wakristo wa Makanisa ya Mashariki, wakati wa kipindi cha Kwaresima kwa kuchangia
kwa hali na mali, ustawi na maendeleo ya watu hawa kiroho na kimwili.
Waamini
na watu wote wenye mapenzi mema wanakumbushwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kwa
Mwaka huu anapenda kuyaelekeza macho yake zaidi huko Syria, Iraq, Misri na Nchi Takatifu,
ili kuhakikisha kwamba, amani na utulivu vinapatikana; watu wanaheshimiwa na kuthaminiwa
utu wao kama binadamu pamoja na kupata mahitaji yao msingi. Waamini wanaweza kuonesha
mshikamano wao kwa kuchangia ustawi na maendeleo ya watu wanaoishi huko Mashariki
ya Kati.
Kardinali Leonardi Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili
ya Makanisa ya Mashariki katika barua yake kwa Maaskofu mahalia anawakumbusha kwamba,
sadaka itakayokusanywa Ijumaa kuu kwa Mwaka 2014 itakuwa ni kwa ajili ya kusaidia
na kuenzi shughuli mbali mbali za kichungaji zinazotekelezwa na Jumuiya za Waamini
katika Nchi Takatifu. Msaada wao wa hali na mali usindikizwe pia kwa njia ya sala.
Ukarabati wa Kanisa la Kuzaliwa Bwana mjini Bethlehemu ni kati ya miradi iliyofanyiwa
kazi kutokana na sadaka iliyokusanywa Ijumaa kuu katika Mwaka 2013. Ukarabati huu
pia umechangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi za kiekumene. Mchango wa Kanisa Katoliki
katika sekta ya elimu bado unahitajika sana anasema Kardinali Sandri. Tatizo la wakimbizi,
wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi ni mambo ambayo pia yanachangiwa na fedha zinazokusanywa
kutoka Majimboni. Watu hawa wengi wao wanaendelea kuhudumiwa na Jumuiya za Kikristo
huko Mashariki ya Kati.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima
anamwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia waamini kutekeleza wajibu wao kwa kuajibika
kikamilifu kwa kuonesha mshikamano wa dhati na wale wote wanaoteseka kutokana na sababu
mbali mbali, ili kuwa kweli ni watu wenye huruma inayomwilishwa kwenye matendo ya
huruma kwa maskini na wahitaji zaidi.
Nchi Takatifu ina kiu ya msaada huu
unaoneshwa na waamini kutoka kwenye Makanisa mahalia, kama kielelezo makini cha imani
tendaji. Mshikamano wa upendo ni kielelezo makini cha maandalizi ya Hija ya Kichungaji
itakayofanywa na Baba Mtakatifu Nchi Takatifu, hii ni hija ya furaha na matumaini
kwa Watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu.