2014-03-01 09:51:53

Majadiliano ni muhimu ili kudumisha haki, amani na utulivu Mashariki ya Kati!


Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni hivi karibuni alifanya hija ya kichungaji nchini Iran na kukazia umuhimu wa viongozi wa dini na serikali kushirikiana kwa pamoja ili kudumisha mchakato unaopania kudumisha misingi ya haki, amani na maendeleo endelevu miongoni mwa watu wanaoishi huko Mashariki ya Kati.

Dr. Tveit anasema, Iran inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa amani na utulivu huko Mashariki ya Kati bila kusahau Syria inayokabiliana na maafa makubwa kwa watu wake. Iran ikiamua kutekeleza wajibu wake kikamilifu katika mchakato wa haki, amani na utulivu, inawezekana kabisa watu kutoka katika imani, makabila na dini tofauti kuishi kwa amani na utulivu.

Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni amekazia pia umuhimu wa kujenga na kuendeleza utamaduni wa majadiliano ya kidini miongoni mwa watu wa imani mbali mbali ili kuheshimiana na kusaidiana kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu.







All the contents on this site are copyrighted ©.