2014-03-01 11:28:24

Leo ni msononoko wa mawazo! Yaani we acha tu!


Katika Injili ya leo Yesu anaanza kwa kusema: Hakuna anayeweza kutumikia mabwana wawili. Mabwana hao anawataja moja kwa moja kuwa ni Mungu na mali. Hiyo mali inaitwa pia Mamonà kutokana na neno la kiebrania mahamuni. Mzizi wa neno hilo mahamuni ni Emuna, au amani - kitu ambacho unaweza kujitegemeza usianguke, kitu ambacho ukikitegemea na kukitumainia kinakupa utulivu na amani. Neno hilo limetoholewa kama lilivyo na kutumika katika lugha ya kiswahili amani, likimaanisha utulivu.

Kadhalika neno mali mzizi wake unatoka katika lugha ya Kiebrania emuna. Hivi unapata pia neno imani, yaani kuaminia, kutegemea, kujiaminisha kwa kitu cha maana kisichokuhadaa au kukudanganya.

Yesu anasema kwamba, hapa duniani kuna vitu viwili vinavyokufanya ujisikie vizuri, utulie, uwe na uhakika, uwe na amani na ukae safi kabisa. Vitu hivyo ni mithili ya, miungu, mabwana au mabosi wawili wanaotupa amri zinazofanana. Moja ya miungu hiyo ndiyo anataja kuwa ni mali ya ulimwengu huu ambayo ni viumbe kama alivyo binadamu, vimeumbwa na Mungu mmoja kwa ajili ya kumtumikia binadamu. Ikitokea kwamba vitu hivyo vinageuzwa kuwa miungu, yaani vinapata ubosi na kuanza kumtawala binadamu badala ya binadamu kuvitawala vitu hivyo, hapo binadamu ataendeshwa na kupata Presha kali.

Miungu hiyo ni kama tunguli za mganga wa chenyeji. Ni vitu vizuri sana, lakini ndiyo vinavyotoa maamuzi ya kitu gani binadamu inabidi afanye. Kumbe Mungu wa kweli aliye mmoja ndiye Bwana, ndiye pekee anayeweza kutoa amri ya kweli yaani, amri ya upendo. Endapo miungu na tunguli ndizo zinazokuamrisha katika maisha yako hapo ndipo litakapokulipukia gonjwa la presha.

Mathalani, endapo pesa ndiyo zinakauwa tunguli zako, bosi wako na mungu wako anayekupa amri utaona kwa mwanzoni ni kitu kizuri sana cha kukuvutia kutaka kuchuma zaidi. Polepole, utapelekeshwa kutaka kuzitamani zaidi. Kama ni nyumba basi utataka kuwa na nyumba nyingi zaidi, kadhalika gari utataka kuwa na gari mpya na la kifahari zaidi, ardhi zaidi nk.

Toka asubuhi hadi jioni akili yako inakuwa imejaa mawazo ya mali. Yesu hakuzuii kuwa na mali, pesa, gari, nyumba nk, anasema: Unao uhuru wako, wa kupenda kutawaliwa na mali ya ulimwengu huu. Lakini kaa chonjo usijidanganye kwamba utakuwa na amani moyoni kwa vile unayo mamona (mali), polepole bila kujitambua utajikuta unayo presha, kwa vile unajikusanyia miungu wengi na unawatolea sadaka zako. Mamona hayo yatakuendesha na kukuamrisha kuwanyonya wanyonge, kuwaonea maskini kwa ajili yako.

Kwa vile utakuwa na lengo moja tu, nalo ni lile la kutaka kufikia malengo yako ya kujitajirisha kwa gharama iwayo yoyote ile, hata ya kuwanyang’anya wengine haki yao. Aidha, hutajua ni kwa nini umepata hiyo presha. Kumbe ni kwa sababu umefika pahali unapokutana na Mungu mwenyewe, sasa kwa sababu ya kumwogopa na ukiunganisha na woga wa kufikiria kufa, hapo unajikusanyia mamona ukidhani utaweza kushinda woga huo. Unashindwa kutambua kwamba maisha ya mwili yana mipaka yake na malengo yake. Endapo Mungu anakuwa Bwana wako basi Yeye atakupa amri za kutumia mali vyema, kwa kupenda wengine na kwa ajili ya maskini.

Injili ya leo inatupendekezea dawa ya kinga na uponyi dhidi ya maambukizi ya presha itokanayo na kuabudu mamona, au mali ya ulimwengu huu, na hatimaye kutupelekea kusahau mipango ya Mungu. Huo ni uponyi wa kuzingatia sana, vinginevyo tunajiharibia maisha ambayo tumebahatika kuyaishi kwa muda huu mfupi wa hapa duniani.

Mungu ametupatia maisha ya ulimwengu huu na yabidi kuyaishi na kuyafurahia ipasavyo na anatutaka tuishi kadiri anavyotaka Yeye. Kwa hiyo ukijipima na kugundua kuwa unayo presha, basi ujue hapo ni ujinga na uzuzu wako ndivyo vilivyokufikisha hadi hapo. Ushauri nasaha na dawa anayotoa Yesu kwa gonjwa namna hii na presha ni kujitambua dhamirini mwako kuwa hapa duniani sisi binadamu ni wahaji na wapita njia tu.

Yesu anaposema: Msisumbuke, msihangaike, Msiwe na presha! Hamaanishi kuwa tusifanye kazi, la hasha, bali tufanye kazi na kuendeleza ulimwengu tulioupewa kadiri ya matakwa yake Yeye aliyeuumba. Yesu anarudia kusema mara sita neno hili msihangaike. Usigeuze shughuli kuwa miungu, hizo zitakupa presha na kukufanya usiweze kufaidi kikamilifu maisha yako hapo duniani. Wewe ni mpita njia tu hapa duniani!

Baada ya ushauri huo nasaha, Yesu anatuletea mifano halisi ya mambo yanayoweza kumhangaisha mtu hadi kumpa presha. Mambo hayo yanahusu kula na kunywa. “Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini” Anataka kutuambia kuwa tusiviruhusu vitu hivyo vitutawale. Tofauti kati ya mtu mwenye imani na yule asiyeamini haiko katika kufanya kazi, kwamba mwamini wa Mungu hafanyi kazi, na yule asiyeamini ndiye anayefanya kazi na kuwa tajiri, la hasha, tofauti ni kwamba yule asiyesadiki anahangaikia, anasumbukia na anataabikia kupata mali kwa ajili yake tu.

Wakati mwamini haangaikii chochote bali anashughulika, anafanya kazi, anasumbuka, anapata taabu katika shughuli, lakini anafanya kazi hiyo ili kupata mahitaji yake na anatambua pia jinsi ya kuwasaidia wengine. Anakuwa bado na utulivu wake wa ndani anapofanya shughuli zake, pindi asiye mwamini anakuwa amejaa mapresha – kisa ni kutafuta kula na kunywa.

Presha nyingine zinapatikana katika kuhangaikia mavazi, ni ile ambayo Yesu anaisemea, “Wala miili yenu, msihangaikie eti mvae nini.” Mavazi yanasaidia kujisitiri, pia kujikinga. Aidha ni alama ya nje inayotambulisha haiba ya mtu yaani, inatuonesha kuwa sisi ni binadamu na siyo wanyama. Aidha, vazi linaonesha kama mtu ni msafi, mtanashati, msomi, mwenye ukwasi, mwenye kipato kupita huyu au yule, na ni mtu wa mitindo gani ya maisha. Kadhalika vazi huitambulisha siku kama ni ya kawaida au ni sikukuu nk.

Kwa hiyo vazi ni kitu huru kabisa anachoweza mtu kujieleza alivyo. Lakini, mavazi yanaweza kugeuka na kuwa miungu na mabosi na kutuendesha hadi kutupatia presha, kwa kujifikiria kuwa mimi si yule mnayemdhania. Hatari hiyo inakuwepo pale mmoja anapotaka kujionesha kuwa ni wa pekee, yaana anayedhani kuwa utu wake unategemea viwalo. Hapo tunapokutana na akina Shabaro, shugamani au masista du! Hao ni wale wanaogharimia kununua mavazi ya bei mbaya ili kuonesha kama wao ni tajiri, wana kazi kubwa, wana vyeo vya maana nk.

Ni sawa na mtu anayenunua pete ya dhahabu inayogharimu mamilioni ya shilingi, au suti ya bei mbaya, au gauni la kutisha. Kila anapoliendea kasha la nguo zake atasimama saa nzima ili kuchagua na kujaribu aina hii au ile ya gauni au suti ya kutokea mbele za watu. Hiyo ni presha.

Baada ya kutoa mifano hiyo halisi, Yesu anatuonesha jinsi alivyo mwanasaikolojia pale anapoamua kututolea kichokoo cha ndege tena ndege wahalibifu anaposema: “Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi gharani, na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je, si bora kupita hao?”

Katika Injili ya kiswahili, ndege wanaotajwa ni mbayuwayu, kumbe ukweli ndege hao walikuwa ni wale waharibifu ambao hawakupendwa kabisa na wakulima kwa vile walikuwa wanakula mazao. Hao tungewalinganisha na ndege wetu ambao kwa lugha ya kingoni wanawaita masokosi, au masweswe na njegeya. Ndege aina hii wanafukua mahindi yaliyopandwa na kula. Wanafaulu hata kuvuna mahindi yaliyokomaa shambani.

Kumbe Mungu anawatunza na kuwalisha hata ndege wa aina hii. Yesu anamalizia tena kutusisitizia, kwamba endapo Mungu anawalisha hata hao ndege mnaowachukia, kwenu si itakuwa zaidi? Kwa hiyo, msipate presha, na kuhangaikia maisha ya kesho. Haya yote wanahangaikia wapagani wasiomjua Mungu. Kesho itajihangaikia yenyewe itakapofika. Wewe ishi leo. Epukana na gonjwa la presha!

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.