2014-03-01 11:08:19

Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani!


Tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa. Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2014 kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli anayewaalika waamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu.

Toba ni kati ya mafundisho ya kwanza yaliyotolewa na Yesu mwenyewe na huu ni mwaliko endelevu unaotolewa na Mama Kanisa kwa watoto wake. Pamoja na mwaliko wote huu, lakini bado Wakristo wengi hawajaweza kumwilisha ujumbe huu katika uhalisia na undani wa maisha yao; ujumbe unaogusa dhamiri, kwani dhana ya dhambi inaonekana kutoweka kwa wengi.

Wongofu unawawajibisha hata watakakatifu ili wasirudie tena nafasi za dhambi na hatimaye kutenda dhambi, tayari kubadilika na kuchuchumilia mambo makubwa na dumifu katika ujenzi wa mahusiano mema na Mwenyezi Mungu pamoja na ulimwengu. Lengo ni kukoleza fadhila ya upendo, unyenyekevu, toba na amani.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, wongofu wa ndani ni hija isiyokuwa na mwisho inayopania kushiriki utakatifu wa maisha ya Kimungu. Ili kufikia lengo hili kuna haja kwa waamini kuwa na mikakati ya maisha ya kiroho inayowawajibisha kubadilika kama anavyosema Mtakatifu Paulo anapowaandikia Wakorintho "Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfao huo huo toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho."

Utakaso wa ndani unapania kusafisha jicho la maisha ya kiroho na hivyo kumwezesha mwamini kujiona kutoka katika undani wake, ili kuwa na roho mpya ya mwana mpendwa wa Mungu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wongofu wa ndani unapaswa kuzaa matunda ya msamaha na mtendo ya huruma kwa jirani; kwa kumpokea na kumwonjesha ukarimu kadiri inavyowezekana pamoja na kumsaidia kupata mahitaji yake msingi. Hiki ni kielelezo cha msingi wa toba ya kweli.

Sehemu ya pili ya utakaso ni kwa waamini kutubu, kuungama dhambi na kujikita katika maisha ya sala katika upendo, unyenyekevu, kwa kushinda ubaya kwa wema; kwa kukimbia nafasi za dhambi na bila kukumbatiwa na malimwengu kwani haya ni chanzo cha kifo cha maisha ya kiroho. Waamini washinde kishawishi cha kiburi na unafiki wa kifarisayo kwa kutambua kwamba, wote ni wadhambi na wanahitaji kuonjeshwa upendo na huruma ya Mungu.

Kipindi cha Kwaresima kinakuja wakati bado kuna watu wanaendelea kukabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa; watu ambao wanapaswa kuonja huruma na mshikamano wa upendo kama kielelezo cha mabadiliko ya ndani na matunda ya toba na wongofu wa kweli. Iwe ni nafasi ya kujinausa kutoka katika dhambi na ubinafsi, kwa kujishikamanisha na Mwenyezi Mungu kwa njia ya fadhila ya unyenyekevu, ili kuomba huruma ya Mungu kama alivyofanya yule Mtoza ushuru aliyehesabiwa haki pale Hekaluni.

Kwaresima kiwe ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya kushiriki mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, si tu kwa njia ya maneno matupu ambayo kamwe "hayawezi kuvunja mfupa" bali kwa njia ya imani tendaji inayoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha. Ni kipindi cha kujishughulisha na maisha mapya yanayofumbatwa katika neema.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, ni fursa kwa waamini kutambua umuhimu wa kutubu, kuongoka na kuchuchumilia wokovu kwa kufanya wongofu wa kweli, kutokana na uwepo wa dhambi walizotenda. Anawatakia kheri na baraka tele katika Kipindi cha Kwaresima.







All the contents on this site are copyrighted ©.