Endelezeni huduma ya huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika kwa namna ya pekee wajumbe wa Chama cha Kitume
cha Mtakatifu Petro kuendelea kuonesha upendo wa Mungu na Kristo kwa njia ya matendo
ya huruma yanayofanywa kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii
na mahujaji wanaomiminika kila siku mjini Roma kwa niaba ya Kanisa.
Ujumbe
wa Baba Mtakatifu Francisko umesomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Georg Ganswen,
Mkuu wa Nyumba ya Kipapa, wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 145 tangu
chama hiki kilipoanzishwa. Mkutano huu umefanyika tarehe 27 Februari 2014. Wajumbe
wamehimizwa kuendeleza matendo ya huruma kwa niaba ya Baba Mtakatifu si tu kwa maskini
na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, bali huduma hii pia iwafikie wagonjwa
na familia zinazokabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na athari za myumbo wa
uchumi kimataifa.
Wajumbe wametakiwa kujielekeza katika kusaidia katekesi
endelevu na kwa vijana wanaojiandaa kwa ajili ya kupokea Ekaristi Takatifu, vituo
vya Katekesi hata kwenye vituo vya mazoezi ya vungo. Yote haya ni makundi yanayohitaji
kuonja huruma na upendo wa Mama Kanisa kwa njia ya huduma za maisha ya kiroho na kimwili.Wajumbe
waonje na kuguswa na mahangaiko ya watu katika medani mbali mbali za maisha.
Rais
Giorgio Napolitano wa Italia kwa kutambua mchango wa Chama cha Kitume cha Mtakatifu
Petro, ametuma ujumbe na matashi mema kwa wajumbe wa mkutano huu, uliowashirikisha
viongozi wakuu wa Kanisa na Serikali ya Italia; wanajeshi na wadau mbali mbali wa
masuala ya mshikamano na utengamano wa kijamii.
Mwishoni wa mkutano huu, wajumbe
wapya walipata nafasi ya kula kiapo pamoja na kuwatunuku nishani wanachama ambao wamedumu
katika Chama hiki kwa kipindi cha miaka ishirini na mitano, kwa kutambua mchango wao
katika kukuza na kuendeleza utamaduni wa mshikamano na upendo kati ya watu.