2014-02-28 08:18:36

Waonjesheni wengine furaha ya kuwa mmissionari!


Furaha ya kuwa mmissionari ndiyo kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya Wahispania kutoka Marekani, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Machi, ili kuonesha moyo wa shukrani kutoka kwa Mama Kanisa kwa ajili ya Mapadre wa Majimbo kutoka Hispania wanaotekeleza wito na utume wao Amerika ya Kusini. RealAudioMP3

Kardinali Marc Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Kanisa la Amerika ya Kusini katika ujumbe wake kwa ajili ya Maadhimisho haya anabainisha kwamba, Mwaka huu, maadhimisho haya yanabeba uzito wa pekee kwani yanafanyika wakati wa uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko, ambaye anatoka eneo la Amerika ya Kusini, changamoto ya kujenga na kuimarisha vifungo vya imani vinavyounganisha Familia ya Mungu kutoka Hispania na Amerika ya Kusini, ili kwa pamoja, waweze kushikamana kwa ajili ya kujitosa kimasomaso katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Kardinali Marc Ouellet anaendelea kusema kwamba, Mwaka 2014u shirikiano wa Mapadre kutoka Hispani na Amerika ya Kusini unaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu ulipoanzishwa. Tangu wakati huo, kumekuwepo na idadi kubwa ya Mapadre waliojimwaga katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Amerika ya Kusini, bila hata ya kujibakiza, Mama Kanisa anawashukuru kwa moyo na majitoleo yao katika kipindi chote hiki cha Miaka 50 ya uwepo wao!

Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa Kitume, Injili ya Furaha anawaalika waamini wote kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha na kuwamegea wengine ile furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake na kwamba, hawana sababu ya kuwa na “uso uliokunjamana kama kigae” kwani ndani mwao wanao utajiri mkubwa ambao ni Imani!

Huu ndio ujumbe wa furaha unaopaswa kusambazwa na Wamissionari wanaotumwa na Mama Kanisa kutangaza Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa watu ambao bado hawajasikia wala kuguswa na Injili ya Furaha. Watu waendelee kutangaziwa Injili ya toba na wongofu wa ndani, ili waweze kubatizwa na hivyo kuwa ni sehemu ya viiungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Familia yote ya Mungu nchini Hispania na Amerika ya Kusini, ijikite katika mchakato wa kuhamasisha, kukuza na kulea miito mitakatifu, ili Kanisa liendelee kupata Wamissionari hodari na watakatifu, tayari kujitosa kwa ajili ya kutangaza Injili ya Furaha.

Kardinali Marc Ouellet anasema kwamba, wakristo wote wanayo kila sababu ya kuboresha ile furaha ya kuwa ni Wamissionari kwa njia ya Ubatizo na kwamba, wanatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu, hata kama bado inaendelea kuwa ni vigumu leo hii kuwa kweli ni Wamissionari wa Injili ya Furaha kutokana na madonda makubwa yaliyojitokeza katika maisha, utume na historia ya Kanisa. Bado kuna watu wanaelemewa na ubinafsi, uvivu na woga wa kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; waamini waliokata tamaa na kujichokea katika maisha ya Kikristo bila kuwasahau wale wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha ya kiimani.

Kutokana na changamoto hizi, Kardinali Marc Ouellet anawaalika Wakristo kuwa karibu zaidi na wote wanaopambana na baa la umaskini wa hali na kipato; njaa na magonjwa; wanaodhulumiwa na kunyanyaswa; familia zinazobaguliwa na kutengwa; watu wanaotumbikia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya, uhalifu wa kutumia silaha; wakanimungu na wote wale ambao kimsingi wamepoteza dira na mwelekeo, hawaoni tena maana ya maisha!

Kuwa mmissionari ina maanisha kusimama kidete na kuwa tayari kujitosa kimasomaso katika mateso na mahangaiko ya watu, kwa kuwa karibu na wote wanaoteseka; wale wanaojitolea kwa ajili ya kuwaonjesha wengine Injili ya Furaha pamoja na kuendelea Kuinjilisha.

Wainjilishaji wakumbuke kwamba, wanapaswa kumshikirisha Roho Mtakatifu kwani ndiye mdau mkuu katika mchakato wa Uinjilishaji, bila msaada wa Roho Mtakatifu, Wamissionari watashindwa kutekeleza dhamana na utume wao kikamilifu, kumbe kuna haja ya kuwa wanyenyekevu na kujikita katika maisha ya sala, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo.

Dhamana ya Kimissionari inatekelezwa kwa kupiga magoti, yaani: kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti; mambo msingi yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mwamini kila siku! Kanisa Amerika ya Kusini lina mchango wa pekee katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, hasa kutokana na uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko. Changamoto iliyoko mbele yao kwa sasa ni kurekebisha mikakati ya kichungaji na miundo mbinu ya Uinjilishaji, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utume wa Kimissionari.

Mwishoni, Kardinali Marc Ouellet, anawakabidhi chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria wa Guadalupe, nyota ya Uinjilishaji Mpya, ili Amerika ya Kusini iweze kutambua na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya kwa kutoka nje ya mipaka ya Amerika ya Kusini, ili kushiriki dhamana na utume wa Uinjilishaji unaotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa.

Wamissionari kutoka Hispania wawe ni mfano na kielelezo cha Umissionari, Ualimu na Wadau wakuu wa dhamana ya utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu; wanaojitahidi kumpeleka Kristo sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili.

Ujumbe huu umehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.