2014-02-28 10:03:21

Vatican kushiriki Expo Milano 2015


Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa niaba ya Vatican ametia sahihi Itifaki ya Ushiriki wa Vatican kwenye Onesho la Expo MIlano 2015, litakalofunguliwa rasmi hapo Mei Mosi, 2015 hadi tarehe 31 Oktoba 2015. Onesho hili litashirikisha nchi zaidi ya 140 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Kulisha Ulimwengu, Nguvu ya Maisha". Dr. Giuseppe Sala, Kamishina wa Expo Milano 2015 ametia sahihi kwa niaba ya Serikali ya Italia.

Banda la Onesho la Vatican litaongozwa na kauli mbiu "Mtu hataishi kwa mkate peke yake", ili kuonesha mwelekeo wa ndani katika maisha ya kiroho na kitamaduni, unaogusa utu na heshima ya binadamu na mahusiano yake katika ngazi mbali mbali anasema Kardinali Gianfranco Ravasi.

Hitaji la chakula ni muhimu sana katika maisha ya binadamu, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kuimarisha mshikamano sanjari na utunzaji bora wa rasilimali ya dunia. Vatican itashiriki kikamilifu kwa kutoa tafakari ya kina kuhusu Lishe katika Onesho la Expo Milano 2015.

Dr. Giuseppe Sala anasema, kuna watu wanaokabiliwa na baa la njaa na ukosefu wa maji safi na salama, changamoto kubwa inayoikabilia Jumuiya ya Kimataifa. Chakula ni sehemu ya haki msingi za binadamu, jambo linalopaswa kutekelezwa kwa kuzingatia uhakika na usalama wa chakula pamoja na maendeleo endelevu. Maonesho haya yanapaswa kuacha alama ya kudumu katika kanuni maadili, ili kukabiliana na changamoto za uhakika wa usalama wa chakula duniani kwa siku za usoni.

Tema kuhusu: baa la njaa, tunu ya maisha, upendo na mshikamano kati ya watu ni mambo yanayohimizwa na Kanisa, kumbe ushiriki wa Vatican kwenye Onesho hili ni muhimu sana na changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kutafuta mbinu mkakati wa kukabiliana na majanga ya maisha.

Banda la Vatican litakuwa na bustani inayopaswa kutunzwa; chakula cha kugawana na wengine; mlo unaofundisha vijana wa kizazi kipya umuhimu wa kuhifadhi chakula pamoja na kuguswa na mahangaiko ya jirani. Mkate utakuwa ni kielelezo cha uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Waamini wanalishwa kwa Chakula cha Neno la Mungu na Mkate wa Uzima wa milele kama mwanzo na kilele cha maisha ya Kikristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.