2014-02-28 10:56:12

Tovuti kwa ajili ya hija ya kichungaji ya Papa Francisko, Nchi Takatifu yazinduliwa


Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kufanya hija ya kichungaji nchini Yordan, Israeli na Palestina kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei, 2014. Kutokana na umuhimu wa tukio hili la kihistoria, viongozi wa Kanisa Katoliki katika Nchi Takatifu wamefungua tovuti itakayowaongoza waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaotaka kufuatilia hija hii ya kihistoria katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene.

Tovuti hii itaweza kusomeka kwa lugha zifuatazo: MKiarabu, Kiebrania, Kiingereza, Kiitaliani, Kihispania, Kireno na Kifaransa. Tovuti hii inafunguliwa kwa picha iliypigwa miaka hamsini iliyopita kati ya Patriaki Athenagora na Papa Paulo VI kunako Mwaka 1964 mjini Yerusalemu. Inafuatia picha kati ya Patriaki Bartolomeo wa kwanza na Baba Mtakatifu Francisko, walipokutana mjini Roma kunako Mwaka 2013.

Tovuti inaelezea kwa kina na mapana lengo la hija ya kichungaji, hali ya maisha na utume wa Wakristo Nchi Takatifu; Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana na Patriaki Athenagora. Ni tovuti inayoonesha Mapapa waliotembelea Nchi Takatifu, Majadiliano ya Kiekumene pamoja na Makanisa mahalia.

Viongozi wa Kanisa Nchi Takatifu kwa kushirikiana na Vatican wameunda Kamati ya Hija ya Kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko itakayomwezesha kukutana, kusali na kuzungumza na Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwenye Kaburi Takatifu. Hiki kitakuwa ni kielele cha Hija ya kichungaji itakayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko. Akiwa mjini Bethelehemu, Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Siku kuu ya Noeli pamoja na Makanisa yote yaliyoko katika eneo hili.

Tume ya mawasiliano inaendelea kujielekeza zaidi katika kuandaa habari kwa ajili ya tukio hili la kihistoria pamoja na kuandaa mazingira yatakayowawezesha wanahabari kutekeleza dhamana yao kwa ufanisi mkubwa wakati wa hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu kwenye Nchi Takatifu. Waandishi wa habari ambao hawatakuwa na vibali vya kushiriki katika msafara wa Baba Mtakatifu wameandaliwa maeneo watakayotekelezea utume wao, kwa kuwapatia habari wanazohitaji kwa ajili ya kazi.

Ukitaka kufahamu kuhusu hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Nchi Takatifu unaweza kufuatilia kwa anuani ifuatayo: www.popefrancisholyland2014.lpj.org







All the contents on this site are copyrighted ©.