2014-02-28 08:02:21

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya VIII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji wa kipindi tafakari masomo Dominika, niko pamoja nawe tena katika Dominika hii ya VIII ya mwaka A wa Kanisa kukushirikisha furaha yangu toka meza ya Neno la Mungu. RealAudioMP3

Mwaliko toka Neno lenyewe ni kwamba kamwe Mungu hawezi kuwasahau watoto wake. Ndiyo kusema kiitikio cha wimbo wa mwanzo kioneshacho tumaini la mzaburi yakwamba Bwana ndiye tegemeo lake daima kinatupa kielelezo murua juu ya upendo wa Mungu kwa watu wake.

Somo la kwanza tunalipata toka Kitabu cha Nabii Isaya ambamo tunamwona Nabii akiwambia Waisraeli watulie na waw na matumaini katika mateso yao. Wanaalikwa kutambua kuwa, pamoja na kwamba wako utumwani Babeli, Mungu ni mkuu na kamwe hataweza kuwaacha katika taabu hiyo. Anawaambia waachane na mantiki ya kuuona utendaji wa Mungu kama utendaji wa mwanadamu ambaye huweza kuwasahau watoto wake. Tunakumbuka katika Israeli kama mmoja aliachana na mke wake haikuwa rahisi tena kurudiana naye, na ilikuwa pia hivyohivyo kama mzazi alimfukuza mtoto wake haikuwa tena ruhusa kumrudisha nyumbani. Ni mambo ya ajabu haya lakini ndo hali ya mwanadamu.

Mpendwa mwana wa Mungu, ni katika mantiki hiyohiyo Waisraeli walipoenda utumwani Babeli kwa sababu ya dhambi na ukaidi wao, walijiona ni kama mwanamke au mtoto aliyefukuzwa nyumbani na hawezi kurudi tena nyumbani. Basi Nabii akitumwa na Mungu anawatuliza akiwakemea kwa sababu ya mawazo yao hayo potofu. Anaweka mbele yao maneno ya Mungu akisema hivi mama aweza kumsahau mwanae anayenyonya? Na hata akimsahau, Mimi Mungu wenu sitaweza kuwasahau ninyi. Mungu anahakikisha ukuu wake na upendo usiopimika kwa maana ya vipimo vya kifalsafa. Mpendwa tukumbuke! “akamtuma Mwanaye wa pekee, akatwaa mwili wetu kwa ajili ya wokovu wetu!!

Katika somo la pili Mt. Paulo anawaandikia Wakorinto akiwaonya na kuwaambia kuwa kuhubiri kwake hakutegemei hekima yake kama binadamu bali hekima ya kimungu. Kumbe anawaomba waelewe kwamba yeye pamoja na wahubiri wengine ni watumishi na wagawaji wa mafumbo ya Mungu. Wakorinto walikuwa na mashaka juu ya mahubiri ya Paulo na hivi kuonesha ukaidi fulani kitu ambacho hivi leo kinazidi kutunyemelea hata sisi watangazaji wa Neno la Mungu. Ukaidi wa Wakorinto ulilala katika mantiki ya kuweka mawazo yao katika wale waliokwishatangulia kuhubiri imani ya Kikristu kwao.

Basi Mt Paulo anakemea hilo na kusema hivi wahubiri ni akina nani? Paulo anazidi kujiuliza hivi Wahubiri wawezaje kuwa ndiyo chanzo cha mgawanyiko katika jumuiya? Ndiyo kusema anataka wahubiri waeleweke kama watumishi wa Neno la Mungu na kwa jinsi hiyo basi, wahubiri si wa kutukuza bali tunaalikwa kumtukuza Mungu. Mpendwa ni katika mantiki hii, kamwe hatutaweza kuwaweka wahubiri mbele na badala yake lazima kumweka Mungu mbele aliye taa ya maisha yetu na kisima cha hekima.

Mpendwa msikilizaji, wewe uliyemhubiri wa Neno la Mungu unaalikwa kuweka neno moja kichwani mwako yaani lile la kupeleka ujumbe wa habari njema kwa uaminifu bila kupunguza kitu wala kuongeza chochote kwa sifa na utukufu wa Mungu. Mt. Paulo anatuangalisha kwa makini katika maisha ya kitume ili kuepuka kuyumbishwa na mawazo potofu yatokayo kwa wale wapokeaji wa mafumbo ya Mungu na pia kuyumbishwa na mawazo yetu sisi wenyewe.

Katika somo la Injili tunakutana na mafundisho ya Bwana ambayo yakazia kuchagua kwa uthabiti kabisa kumtumikia Mungu au kutumikia mali. Ndiyo kusema haitawezekana kumtumikia Mungu na wakati huohuo ukitumikia miungu inayowakilishwa na mali au fedha. Bwana anasema yatupasa kuwa makini akitoa mfano rahisi lakini ulio na uzito! Anasema hivi hata ukihangaika kwa ukitafuta mali waweza kujiongezea kimo chako? Asema tena Je,? kama maua ya kondeni Mungu ayafanya yapendeze hivi je kwetu sisi watoto wake wapendwa, hatafanya zaidi?, kwa nini tunajihangaisha? Baada ya maswali haya, Bwana anasema “tafuteni kwanza ufalme wa mbingu mengine yote mtayapewa kwa ziada”! Mpendwa msikilizaji, ndiyo kusema, Mungu hatatuacha wala kutusahau bali yuko pamoja nasi.

Mpendwa msikilizaji, yafaa kujiuliza kidogo hivi hatari ya fedha au mali yamnyemelea nani? Wa hakika hatari hii inawanyemelea matajiri na maskini kwa ujumla wao. Kumbuka amri ya ya kwanza ya Mungu, inayoelekezwa kwa wote maskini na tajiri ikisema, ndimi Bwana Mungu wako usiabudu miungu wengine. Kut. 20:3. Kwa hivi mpendwa msikilizaji lazima kuwa makini tusije kuanguka katika falisafa ya kuwatazama matajiri kama ndio wanaoguswa na jambo hili. Tukisonga mbele katika tafakari tunajiuliza tena, hivi mali yawezaje kuwa muungu wakati ni kitu cha kugusika? Kwa hakika mali hugeuka na kuwa muungu wakati tunapoweka mawazo yetu katika mali hiyohiyo!

Katika hili tunasaidiwa kuelewa tunapokumbuka wajibu wetu wa kumpenda Mungu kwa akili na kwa mawazo yetu yote!! Mpendwa mwana wa Mungu yafaa kujiuliza hivi katika Biblia miungu yatajwa kwa majina gani? Kwa hakika katika Biblia tunakutana na miungu midogo kama vinywaji vinavyotupeleka katika ulevi, fedha, uasherati, tabia fulani katika tamaduni zetu nk. Mwaliko kwetu ni kuwa makini kupambana na vinyemelezi hivi katika maisha yetu.

Katika Injili ya Dominika hii kile kinchotajwa kama mungu ni fedha. Tunajiuliza kwa nini fedha wakati fedha tunatambua ni kwa ajili ya mabadilishano? Fedha inakuwa kiwakilishi cha miungu kwa sababu kama mtu aliyenazo si mwadilifu aweza kujipatia kila aina ya kitu kinyume na hali ya kawaida. Mtu huyo aweza kufanya safari haramu, aweza kununua kura haramu, aweza kula na kusaza na kutupa chakula, aweza kuwahonga wasimamizi wa hifadhi za taifa na kupora tembo na mambo kama hayo. Ndiyo kusema polepole ndani ya mtu hukua na kukomaa mawazo kinyume na utu wa kawaida.

Ni katika kukomaa kwa mawazo haya mtu huweza kuacha hata mke wake au mme wake, huweza kuacha watoto wake katika taabu, huweza kusahau masilahi ya taifa lake, huweza hata kuua katika mantiki ya kujilinda na mambo kama hayo. Huu ndio muungu, ndio uondoaji wa heshima na uhuru kwa mtu mwenye fedha na mawazo ya fedha na mali kwa ujumla.

Mpendwa msikilizaji yafaa kujiuliza swali jingine, hivi ni kwa nini Mungu na fedha au mali si rahisi kukaa pamoja? Kwa hakika fedha au mali anayo falisafa ya kuongeza mali na fedha kwa namna yoyote. Matokeo ya hili ni kuwanyonya maskini na hata kuwatupilia mbali. Ni kuwanyima dawa wanaougua, ni kuwapiga na kuwajeruhi wale wanaodai haki kwa ajili ya masilahi ya taifa na jumuiya kwa ujumla. Kama ni wapangaji wake wa nyumba, basi mali ataka walipe hata kwa udi na uvumba vinginevyo ni kuwatoa nje ya nyumba, tena zaidi ongezeko la kodi bila utaratibu!

Wakati mali akisisitiza falisafa ya ongezeko la mali, Mungu asisitiza na kurudia kinyume cha mali akisema mpende jirani yako, heri walio maskini wa roho, heri wanaothamini masilahi ya taifa na watu, msaidie mwenye shida na mfunge vidonda mwenye taabu kama alivyofanya Msamaria mwema na hapa kuna maisha na tuzo ya uzima. Hizi falsafa mbili haziwezi kukaa pamoja, kumbe mwanadamu lazima achague kuishi! yaani falisafa ya upendo kwa Mungu na kwa watu.

Sehemu ya pili ya Injili inatukumbusha kuwa watu wa kujenga amani moyoni, yaani, kumtegemea Mungu daima. Kumbuka wimbo wetu usemao “palipo na mapendo hapo Mungu yupo” maana yake tujishughulishe na shughuli za upendo na Mungu atakuwa nasi daima. Mpendwa yafaa kuwa makini sana tunapoisoma Injili hii, maana mwanzoni mwa sehemu ya pili inasema msijihangaishe mtakula nini, angalieni maua ya kondeni na ndege wa angani.

Kumbe yaweza kupelekea tukaacha kufanya kazi! Kwa hakika Bwana apenda tuwajibike, kumbe Injili haisemi msifanye kazi bali inasema msiwe na wasiwasi, ndiyo kusema wakati mkifanya kazi mtegemee Mungu na yote yataenda. Narudia kusema Mungu ataka tuwe na utulivu na amani moyoni mwetu lilillo tunda la Roho Mtakatifu na si tuwe wavivu na wajanja wa mtaani!

Mpendwa mwana wa Mungu, tunaalikwa kuwa na amani kwa sababu maisha yetu yako ndani ya moyo wa Mungu. “yeye aliyeanzisha kazi yake ajua kuiendeleza”-Mtakatifu Gaspari. Ndiyo kusema, unaalikwa kutambua kuwa kazi yoyote njema ukiikabidhi mikononi mwa Mungu itafaulu daima. Aidha Mungu habezi mali bali akataa mali kuchukua nafasi ya Mungu. Ndiyo kusema mali iwe kwa ajili ya kumtumikia yeye. Tumia na zalisha mali kwa kuwasaidia watu wa Mungu: jenga shule, anzisha vituo vya yatima, saidia watu wanaohitaji msaada wa kisheria na tumia mali kujenga ustawi wa familia yako na kukomaza mapendo kwa watu na Mungu.
Mpendwa ninakutakia furaha na matumaini katika maisha yako daima ukimtanguliza Mungu na kwa namna hiyo kuijua hekima ya kweli itokayo kwa Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.