Papa Francisko achambua uzuri na utakatifu wa ndoa
Uzuri na utakatifu wa maisha ya Sakramenti ya Ndoa unaweza kueleweka vyema zaidi kwa
kufanya rejea kwa Kristo na Kanisa lake. Wana ndoa katika shida na mahangaiko yao
ya ndani wanapaswa kusaidiwa na wala si kuhukumiwa na kwamba, Yesu Kristo ndiye Mchumba
mwaminifu wa Kanisa lake. Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri
yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe
28 Februari 2014.
Mafarisayo na Walimu wa Sheria walitaka kumpokonya Yesu mamlaka
yake ya kimaadili kwa kumtega na swali kuhusu ndoa na talaka. Ni swali linaolenga
kuvuruga uhusiano kati ya Mungu na binadamu na kati ya wanandoa, lakini Yesu anawakumbusha
kwamba, tangu mwanzo Mwenyezi Mungu alimuumba mwanaume na mwanamke wanaounda familia
na kuwa ni kitu kimoja. Muungano huu kati ya mwanaume na mwanamke unaonesha utukufu
wa Mungu katika kazi ya Uumbaji.
Mwenyezi Mungu anampatia Adamu mwenza wa hija
ya maisha; upendo unaoendelea kujionesha katika maisha ya mwanadamu, hata pale mwanadamu
aliposhindwa kuwa mwaminifu, lakini bado Mwenyezi Mungu aliendelea kumwonjesha upendo
usiokuwa na kifani! Upendo kati ya Kristo na Kanisa lake unafafanuliwa vyema na Mtakatifu
Paulo katika Nyaraka zake. Huu ndio ule uhusiano kati ya Mungu na Waisraeli katika
Agano la Kale; Kristo na Kanisa lake katika Agano Jipya.
Baba Mtakatifu anawaalika
waamini na watu wenye mapenzi mema kusikia uchungu pale pendo linapovurugika na kuingia
mchanga, mwaliko wa kuwasindikiza wale ambao pendo lao limemeguka badala ya kuwalaani
na kuwakashfu. Hii ndiyo sheria ya upendo wa Kikristo kwa wanandoa kadiri ya Mpango
wa Mungu unaowashirikisha katika kazi ya Uumbaji.
Huu ndio uzuri wa maisha
ya ndoa na familia ya Kikristo, changamoto na mwaliko wa kuwaenzi wanandoa katika
hija ya maisha yao ya ndoa na familia. Kwa wanandoa ambao upendo wao umemeguka wasaidiwe
kuonja tena upendo wa Kristo na Kanisa lake. Wanandoa wajifunze kushinda kishawishi
cha kutalakiana; watambue kwamba, ndoa ni upendo dumifu hadi kifo kitakapowatenganisha.