Papa akutana na viongozi wa kidini kutoka Argentina
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni tarehe 27 Februari 2014 amekutana na kuzungumza
na Kikundi cha viongozi 45, kutoka dini ya Kiislam, Kiyahudi na Kikatoliki kutoka
Argentina, waliokuwa wanarejea kutoka katika hija ya maisha ya kiroho katika Nchi
Takatifu.
Viongozi hawa wametembelea katika maeneo ambayo Baba Mtakatifu Francisko
katika hija yake ya kichungaji Nchi Takatifu ataifanya, yaani Yordani, Israeli na
Palestina. Viongozi hawa wamekutana na kuzungumza na viongozi wa kidini na kisiasa
katika maeneo haya.
Hiki ni kikundi cha viongozi wa kidini ambacho bado kinaendeleza
ushirikiano na Baba Mtakatifu Francisko katika msingi wa maisha ya kiroho, ndiyo maana
viongozi hawa wamehitimisha hija yao ya maisha ya kiroho kwa kukutana na kuzungumza
na Baba Mtakatifu Francisko.
Mkutano huu umehudhuriwa pia na viongozi wa Baraza
la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo pamoja na Baraza la Kipapa la Majadiliano
ya Kidini. Hayo yamefafanuliwa na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican.