Majandokasisi wa Jimbo kuu la Roma wanasubiri kwa hamu kukutana na kuzungumza na Papa
Francisko
Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Bikira Maria, Mama wa
Imani, Msimamizi wa Jumuiya Seminari ya Jimbo kuu la Roma, Ijumaa jioni tarehe 28
Februari 2014 anatarajiwa kutembelea na kuzungumza na Waseminari wa Seminari kuu ya
Jimbo kuu la Roma, kwenye Eneo la Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano, kilichoko mjini
Roma.
Huu utakuwa ni mwanzo wa Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka Mia Moja tangu
Bikira Maria Mama wa Imani alipochaguliwa kuwa Msimamizi wa Jumuiya hii ya malezi
kwa Jimbo kuu la Roma. Tarehe Mosi, Machi, 2014, Kardinali Agustino Vallini, Makamu
Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu majira
ya asubuhi kama sehemu ya Maadhimisho haya.
Itakuwa ni mara ya kwanza kwa Baba
Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na Jumuiya ya Malezi ya Jimbo kuu la Roma
ambayo kwa sasa ina jumla ya Waseminari 80 pamoja na walezi wao. Mkutano huu wa Baba
Mtakatifu utawajumuisha pia na Waseminari kutoka Seminari zilizoko mjini Roma pamoja
na kujibu maswali yatakayoulizwa na Majandokasisi. Baba Mtakatifu Francisko atahitimisha
mkutano huu kwa kupata chakula cha usiku pamoja na Jumuiya nzima ya Seminari kuu ya
Jimbo kuu la Roma.