2014-02-27 08:23:52

Maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia yapamba moto!


Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu, hivi karibuni, imehitimisha mkutano wake wa kumi na tatu, uliofanyika katika kipindi cha siku mbili. Mkutano huu umejadili pamoja na mambo mengine, majibu ya maswali dodoso yaliyotumwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki duniani kote kama sehemu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayoadhimishwa mjini Vatican mwezi Oktoba, 2014.

Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia ya majibu yaliyotolewa ni kubwa na kwamba, kumekuwepo pia na majibu yaliyotolewa na makundi pamoja na watu binafsi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kikao cha Sekretarieti, kilihudhuriwa pia na Baba Mtakatifu Francisko aliyekazia kwa mara nyingine tena umuhimu wa Sinodi kama kielelezo makini cha umoja na mshikamano wa Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia sanjari na mada itakayojadiliwa kwenye Sinodi ya Mwaka 2014 na ile ya Mwaka 2015.

Wajumbe wamefurahia majibu ya dodoso ya maswali yaliyoulizwa na kwamba, hapa patakuwa ni mahali ambapo sauti ya Makanisa mahalia itaweza kusikika mintarafu: maisha, utume, matatizo na changamoto za maisha ya ndoa na familia; tayari kutweka hadi kilindini ili kutangaza Injili ya Familia, licha ya changamoto na kinzani zinazojitokeza katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Majadiliano haya yatasaidia katika utengenezaji wa Hati ya Kufanyia Kazi inayojulikana kwa lugha ya Kilatini kama "Instrumentum Laboris". Kuna uhusiano wa dhati kati ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kuhusu Familia na Sinodi ya Kawaida ya Maaskofu kuhusu Familia, Sinodi ambayo itatoa mapendekezo yatakayotumiwa na Baba Mtakatifu katika kuandaa Waraka wake wa Kitume kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu.

Mkutano huu umehudhuriwa pia na Wawezeshaji wakuu wa Sinodi: Kardinali Peter Erdo pamoja na Askofu mkuu Bruno Forte, Katibu maalum wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia. Baba Mtakatifu Francisko alitumia fursa hii kubariki eneo jipya la Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu ambayo kwa sasa ina Kikanisa na Ofisi mpya ili kurahisisha utekelezaji wa shughuli za Sinodi za Maaskofu.







All the contents on this site are copyrighted ©.