2014-02-27 11:41:55

Kashfa zinaua maisha ya watu!


Mwamini anayeimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara anapaswa kutolea ushuhuda wa imani yake kwa Kristo na Kanisa lake pasi na woga wala makunyanzi. Mwamini ambaye kweli ni mfuasi wa Kristo anafikiri na kutenda kadiri ya Kristo mwenyewe, hali inayoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha. Kama hakuna ushuhuda wa maisha ya Kikristo hapo kuna jambo ambalo haliendi sawa sawa na linapaswa kushughulikiwa kikamilifu.

Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican siku ya Alhamisi. Anasema, wakristo wanaoshindwa kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, hawalitendei vyema Kanisa. Watu wanaotumia mali na utajiri wao vibaya kwa ajili ya kuwadhulumu na kuwanyanyasa maskini na wanyonge wanakwenda kinyume cha Mafundisho ya Kristo na kwamba, kilio na mahangaiko ya watu hawa iko siku yatasikika mbele ya Mwenyezi Mungu na wahusika watakiona cha mtema kuni! Anasa na tamaa za mwili yamekuwa ni mambo yanayowafurahisha wengi lakini yanakwenda kinyume kabisa na njia za Bwana. Hii ni kashfa.

Yesu katika Mafundisho yake anakemea kwa ukali kashfa dhidi ya wadogo wanaomwamini na kwamba, kashfa zinamwelekeo wa kuua maisha ya watu kiroho. Kuna haja anasema Baba Mtakatifu Francisko kuhakikisha kwamba, maneno na matendo ya Wakristo yanashuhudiwa katika uhalisia wa maisha na wala si kinyume chake. Imani ijioneshe katika matendo. Ushuhuda wa imani tendaji ni kikolezo hata kwa wale wasioamini.

Baba Mtakatifu anasema, kwa mtu asiye amini anavutwa zaidi na ushuhuda wa matendo yanayoonesha mambo makuu yanayofumbatwa katika moyo wa mwanadamu. Imani bila matendo, hiyo imekufa ndani mwake, hata kama mwamini atadiriki kusimulia Biblia nzima kwa mtu asiye amini, bila matendo ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa! Wakristo waoneshe ushuhuda wa imani tendaji, hapo mambo yataweza kubadilika.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali ili kuwaombea waamini waweze kutolea ushuhuda wa imani yao katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Pale waamini wanapojikuta wanaogelea katika dimbwi la dhambi na mauti, wasisite kukimbilia upendo na huruma ya Mungu. Wakristo waoneshe ujasiri wa kutubu na kumwongokea Mungu!







All the contents on this site are copyrighted ©.