2014-02-27 12:14:58

Jengeni utamaduni wa kuheshimiana, kuthaminiana na kupendana, ili haki, amani na utulivu viweze kushamiri!


Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu, changamoto kubwa inayomkabilia binadamu ni kupendana, kuheshimiana na kusaidiana kwa hali na mali. Kukosa na kukoseana ni jambo la kawaida katika hija ya maisha ya binadamu, lakini kuanza kulipiza kisasi ni kwenda kinyume kabisa cha mpango wa Mungu kwani kimsingi mwanadamu anakosa vigezo vya kutekeleza haki kadiri ya mpango wa Mungu.

Kutokana na ukweli huu, mwanadamu hana budi kuhakikisha kwamba, anaachana na tabia ya kulipiza kisasi. Mwenyezi Mungu amewaumba binadamu katika tofauti kubwa, lakini wote wanapaswa kuishi kama Jumuiya kwa kusaidiana, kwani hakuna mtu anayeweza kuishi kama kisiwa. Wakristo kwa namna ya pekee wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha mshikamano wa upendo kati yao na wale wote wanaowazunguka, ili kupandikiza mbegu ya haki, amani na upatanisho wa kweli unaobubujika kutoka katika undani wa mtu!

Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu msaidizi Titus Mdoe wa jimbo kuu la Dar es Salaam katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Bikira Maria wa Consolata, Kigamboni. Askofu msaidizi Mdoe alikuwa Parokiani hapo ili kutembelea na kuzungumza na Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Ushuhuda wa maisha adili na amini uwe ni mfano wa kuigwa na jirani wengine. Upendo kwa Mungu na jirani ni silaha madhubuti dhidi ya vita, kinzani na migogoro ya kijamii inayoendelea kufuka moshi sehemu mbali mbali za dunia na kama inavyojionesha pia nchini Tanzania.

Askofu msaidizi Titus Mdoe anasema kamwe watu hawawezi kulingana, watatofautiana, lakini hawana budi kujenga na kuimarisha utamaduni wa kupendana na kusaidiana kwa hali na mali kama ndugu wamoja. Kuna watu wanaokabiliana na hali ngumu ya maisha ndani ya Jamii wakati huo huo kuna kundi la watu wachache wanaoendelea kuvinjari na kuponda maisha.

Waamini wanahamasishwa kujenga moyo wa kusamehe na kusahau, ili kuanza mchakato wa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, ili kujenga mazingira yatakayoiwezesha dunia kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Watu wajitaabishe kufanya kazi halali ili kujipatia mahitaji yao msingi na kwamba, hakuna njia ya mkato katika maisha kwa kujikita katika imani za kishirikina zinazoendelea kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Utajiri unapatikana kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Chuki na uhasama wa kisiasa ni sumu inayoweza kukwamisha maendeleo ya watanzania wengi. Kumbe, watanzania hawana budi kuhakikisha kwamba, wanaondokana na siasa zinazojenga chuki na uhasama kati yao. Waongozwe na hoja ya nguvu na wala si nguvu ya hoja kama inavyojionesha katika mikutano mingi ya kisiasa.

Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea mjini Dodoma watambue dhamana kubwa waliyopewa na watanzania wenzao katika mchakato wa kutafuta Katiba itakayokuwa ni Sheria Mama katika utekelezaji wa haki msingi za binadamu, demokrasia na uhuru wa kweli; utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ustawi na maendeleo ya watanzania wote yapewe kipaumbele cha kwanza badala ya kuangalia makundi ya watu wanayoyawakilisha kwenye Bunge hili maalum.

Na Rodrick Minja,
Dodoma







All the contents on this site are copyrighted ©.