2014-02-27 09:45:34

Imani za kishirikina ni chanzo cha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia!


Tume ya haki na amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon inawakumbusha waamini na wananchi wa Gabon katika ujumla wao kwamba, maisha ya mwanadamu ni matakatifu yanapaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa na kutunzwa. Inasiktisha kuona kwamba, kuna baadhi ya watu wenye uchu wa mali na madaraka wanachezea maisha ya mwanadamu kwa njia ya mauaji ya watoto wasiokuwa na hatia kama kafara, mambo yanayoendeleza imani za kishirikina. RealAudioMP3

Hata katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, bado kuna watu wanaendelea kudanganywa kwamba, wanaweza kupata utajiri wa haraka haraka na madaraka kwa njia ya mkato, yaani kwa njia ya waganga wa kienyeji wanaoendelea kusababisha majanga ndani ya Jamii. Umefika wakati kwa wananchi wa Gabon kujitafutia maendeleo, mali na madaraka kwa njia halali na wala si kwa njia za kishirikina.

Askofu Jean Vincent Ondo Eyene ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa Maadhimisho ya Siku ya pili ya kitaifa kwa ajili ya kuombea amani na utulivu nchini Gabon pamoja na kuwakumbuka watoto ambao wameuwawa kikatili kwa ajili ya kutolewa kafara na watu wanaoendelea kukumbatia imani za kishirikina. Maaskofu wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujipatanisha na Kristo anayewachangamotisha kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani na upatanisho.

Kwa ujio wa Kristo, ile sheria ya jino kwa jino au jicho kwa jicho imepoteza dir ana mwelekeo na badala yake watu wanafundishwa kumpenda Mungu na jirani zao, lakini zaidi ya hayo, kuwapenda na kuwaombea hata adui zao. Gabon ni kati ya nchi za Kiafrika zinazoendelea kujikita katika mchakato wa kuwaletea watu wake maendeleo, lakini kwa bahati mbaya sera za Serikali zinajikita katika maendeleo ya kiuchumi na kusahau utu na heshima ya binadamu.

Ikumbukwe kwamba, mwanadamu anapaswa kuendelezwa kiroho na kimwili na ndiyo maana Kanisa linaendelea kujikita katika Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Maaskofu wa Gabon wanasema, kilio cha maendeleo endelevu yanayomgusa mtu mzima, unaonekana kana kwamba ni wimbo usiokuwa na kiitikio!

Dhana, sera na mikakati ya maendeleo inajikita zaidi katika mambo yanayoathiri utu na heshima ya binadamu. Watu wanatafuta mali kwa ud ina uvumba, kiasi hata cha kuwatoa ndugu zao kafara. Imani za kishirikina zinaendelea kuhatarisha maisha ya watu wasiokuwa na hatia nchini Gabon. Kuna watu waliokamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya mauaji kutokana na imani za kishirikina hadi leo hii wanaendelea “kutesa na kutamba mitaani kana kwamba, wale waliouwawa hawana thamani mbele ya Jamii”.

Maaskofu wanasema, familia nyingi zinangoja kuona haki inatendeka, wahusika wa mauaji ya watu wasiokuwa na hatia wanafikishwa mbele ya mkondo wa sheria na sheria kweli ifanye kazi yake. Serikali ijikite zaidi katika mapambano ya baa la umaskini, ujinga na maradhi. Watu waelimishwe umuhimu wa kufanya kazi halali ili kujipatia kipato cha halali na kwamba, katika maisha hakuna njia ya mkato! Tume ya haki na amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon inasema, haki itendeke na maisha ya binadamu yaheshimiwe!








All the contents on this site are copyrighted ©.