Askari watoto wanaopelekwa mstari wa mbele kupigana ni kati ya changamoto kubwa iliyoko
mbele ya Jumuiya ya Kimataifa. Hili ni kundi ambalo linaishi katika mazingira hatarishi
pamoja na kuaminishwa kupata mambo makubwa hata pengine kinyume kabisa cha umri wao.
Ni watoto wanaofundishwa kuvuta bangi katika umri mdogo, kuanza tabia chafu ya kubaka
wasichana na wanawake pamoja na kuua bila huruma.
Askari yoyote
mwenye umri chini ya miaka kumi na minane kadiri ya sheria za Umoja wa Mataifa anahesabiwa
kuwa bado ni mtoto na haruhusiwi kushiriki katika masuala ya kivita, lakini ukweli
wa mambo ni kwamba, kuna watoto zaidi ya laki tatu ambao wako mstari wa mbele. Hii
inatokana na uzoefu unaoonesha kwamba, kuwatunza watoto ndani ya Jeshi ni rahisi kwani
wao wanahitaji chakula kidogo tu na ni wepesi kushika na kutekeleza amri kutoka kwa
wakuu wao.
Ni kundi linalofanyishwa kazi za suluba kama vile: kubeba mizigo,
kupika na kuwateka wanawake na wasichana. Hii ni taarifa iliyotolewa hivi karibuni
na Shirika la Wasalesiani huko Madrid, Hispania. Taarifa za Umoja wa Mataifa zinazonesha
kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2013 kuna makundi hamsini ya majeshi ya waasi na
kuna mataifa manane yanayoendelea kuwafunza watoto kushika silaha kinyume cha sheria
na kanuni za Umoja wa Mataifa.
Pale ambapo kuna kinzani na migogoro ya kivita,
watoto na vijana ni rasilimali watu ya kwanza kabisa kutafutwa na kutumiwa, kama inavyojionesha
katika nchi ambazo zina vita na migogoro ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia. Kuna
kundi kubwa la watoto na vijana linalopokonywa matumaini ya maisha bora zaidi kutoka
katika familia zao kwa kulazimika kwenda mstari wa mbele ili kupigana vita!
Mambo
makuu yanayowatumbukiza watoto katika vita na majanga mengine ya maisha ni pamoja
na: umaskini na hali ngumu wanayokabiliana nayo, kiasi hata cha kukata tamaa na hivyo
kukosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha. Baadhi ya watoto hawa ni wale wanaotoka
katika familia zilizotengana, watoto waliodhalilishwa utu na heshima yao, watoto ambao
wameacha shule au ambao wakati mwingine wametekwa nyara. Kuna haja kwa Jumuiya ya
Kimataifa kusimama kidete kupinga unyanyasaji wa watoto kwa kupelekwa mstari wa mbele!