2014-02-25 14:36:03

Simameni kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani, demokrasia, maadili na utu wema!


Miaka ishirini ya Demokrasia imekwisha gota, Familia ya Mungu pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Afrika ya Kusini wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi kubwa ya demokrasia nchini Afrika ya Kusini. Hiki kiwe ni kipindi muafaka kwa ajili ya maandalizi makini ya Uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Afrika ya Kusini tarehe 7 Mei 2014. RealAudioMP3

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini katika barua yake ya kichungaji kuelekea kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Afrika ya Kusini, linawaalika waamini na wananchi wote wenye mapenzi mema nchini Afrika ya Kusini kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani, demokrasia, maadili na utu wema.

Ni wakati wa kufutilia mbali kasoro zilizojitokeza wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika ya Kusini, sanjari na kuendeleza maboresho ya maisha ya wananchi wengi wa Afrika ya Kusini wanaoendelea kuteseka kutoka na umaskini wa hali na kipato. Serikali iendelee kuwekeza katika ukuaji wa uchumi, maboresho ya miundo mbinu na huduma msingi kwa wananchi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linabainisha kwamba, miaka ishirini ya demokrasia imekwisha yoyoma, lakini bado kuna cheche za ubaguzi wa rangi, dhuluma na nyanyaso kwa watoto wadogo, kuna mamillioni ya watu bado wanaandamwa na umaskini mkubwa, magonjwa na ujinga; ujambawazi na matumizi ya nguvu bado ni matukio yanayochafua amani na utulivu nchini Afrika ya Kusini.

Maaskofu wa Afrika ya Kusini wanawachangamotisha waamini kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya Injili kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, biashara haramu ya dawa za kulevya na binadamu pamoja na utumwa mamboleo vinakomeshwa nchini Afrika ya Kusini.

Maaskofu wanawataka wanasiasa na wananchi wa Afrika ya Kusini katika ujumla wao kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kwa kujikita katika misingi ya ukweli, uwazi na uwajibikaji, kwa kuheshimiana na kusaidiana, kwani kimsingi wananchi wote wa Afrika ya Kusini ni ndugu wamoja. Serikali inapaswa kutumia rasilimali ya nchi kwa ajili ya mafao ya wengi.

Vikosi vya ulinzi na usalama viwe mstari wa mbele kuwalinda raia na mali zao; waalimu wajielekeze zaidi kutoa elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya na wazazi wawe waalimu wa kwanza wa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu na kwamba, ni wajibu wa viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Afrika ya Kusini: kiroho na kimwili kwa njia ya huduma makini!

Baraza la Maaskofu wa Afrika ya Kusini linasema, mchakato wa demokrasi nchini humo unawahusu na kuwagusa wananchi wote wa Afrika ya Kusini na wala si tu jukumu la wanasiasa wachache ndani ya Jamii. Kila mwananchi wa Afrika ya Kusini anapaswa kuchangia kwa hali na mali maendeleo na ustawi wa nchi yake.

Kuhusiana na uchaguzi mkuu nchini Afrika ya Kusini, Maaskofu wanawaomba wananchi kuhakikisha kwamba, wanawapigia kura viongozi wa kisiasa wanaosimama kidete kulinda na kutetea utakatifu wa maisha ya mwanadamu; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; watu wanaowajibika, tayari kutoa kipaumbele kwa ajili ya mafao ya wengi; watu wanaojibidisha kwa ajili ya kujenga na kudumisha umoja, upendo, usawa na mshikamano wa kitaifa, bila kuwasahau maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Sera za vyama vya kisiasa hazina budi kujielekeza katika mchakato wa maboresho ya huduma makini za kijamii. Ukabila, udini, rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma havina nafasi kwa ujenzi wa dekomrasia ya kweli nchini Afrika ya Kusini wanasema Maaskofu.

Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linawaalika waamini na wanchi wote wa Afrika ya Kusini kumshukuru Mungu kwa zawadi ya demokrasia katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita. Waamini waendelee kusali kwa ajili ya kuiombea nchi yao, ili watu waweze kuwa na matumaini, amani, umoja, upendo na mshikamano wa dhati.

Imeandaliwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.