Papa Francisko aunda Taasisi za kusimamia na kuratibu shughuli za uchumi na fedha
ya Kanisa
Mama Kanisa amepewa dhamana ya kusimamia kwa uaminifu na busara mali ambayo amekabidhiwa
kama sehemu ya utekelezaji wa utume wake wa Uinjilishaji, kwa kutoa kipaumbele cha
kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.Usimamizi na uratibu
mzuri wa mali ya Vatican una uhusiano wa pekee na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro
kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu sanjari na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Kwa
maneno haya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 24 Februari 2014 ameanzisha
muundo mpya wa uchumi na uratibu wa shughuli za Vatican, baada ya kufanya marekebisho
makubwa kuhusiana na Waraka wa Kitume wa Mchungaji Mwema, Pastor Bonus. Baada ya kupokea
ushauri wa Makardinali kwa hiyari yake mwenyewe ameamua kuunda Baraza la Kipapa la
Uchumi litakalosimamia na kuratibu shughuli zote za uchumi na fedha mjini Vatican
pamoja na kusimamia taasisi zote zilizoko chini ya Vatican.
Baraza la Kipapa
la Uchumi litakuwa na wajumbe kumi na watano, kati yao kutakuwepo na Makardinali au
Maaskofu wanane watakaoteuliwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kama kielelezo
cha uwakilishi wa Kanisa la Kiulimwengu, wajumbe wengine saba watakuwa ni wataalam
walei watakaoteuliwa kutoka katika mataifa mbali mbali: hawa wanapaswa kuwa na sifa,
ujuzi na weledi katika masuala ya fedha na uchumi.
Baraza la Kipapa la Uchumi
litasimamiwa na Kardinali ambaye atakuwa na dhamana ya kuratibu shughuli zote.
Baba
Mtakatifu Francisko ameunda pia Sekretarieti ya Uchumi itakayokuwa inawajibika moja
kwa moja kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kuunda
sera, kanuni na taratibu za manunuzi sanjari na ugavi bora wa rasilimali watu kwa
kuzingatia mahitaji ya taasisi husika. Sekretarieti ya Uchumi itasimamiwa na Kardinali,
kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Vatican na kwamba, Katibu mkuu wa Sekretarieti
atakuwa na dhamana ya kumsaidia Kardinali ambaye ataratibu shughuli zote hizi.