Inasikitisha kuona umati mkubwa wa watoto wanakufa kwa njaa na utapiamlo kwenye kambi
za wakimbizi, wakati ambapo watengenezaji na wafanyabiashara ya silaha wanaendelea
kuponda maisha. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha misingi ya
haki, amani, upendo na mshikamano.
Kamwe watu wasikubali vita kuwa ni sehemu
ya mazoea yao na mambo yanayopamba taarifa za vyombo vya habari kwani hii ni kashfa
kwa watu wa nyakati hizi: wivu na tamaa ya madaraka na utajiri wa haraka haraka ni
kati ya mambo yanayochangia kuenea kwa vita sehemu mbali mbali za dunia. Watu wamekosa
fadhila ya unyenyekevu na majadiliano na matokeo yake wanataka kuheshimiwa na kuabudiwa,
matokeo yake ni vita na kinzani za kijamii.
Vita kwa sasa imekuwa ni kati ya
mambo ya kawaida. Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka inafanya kumbu kumbu ya vita kuu
ya dunia, lakini leo hii kuna vita inayoendelea katika mataifa mbali mbali lakini
hakuna mtu anayekwazika. Ndugu wanauwana kutokana na wivu, ubaguzi wa kikabila, vita
na uchu wa mali na madaraka. Watu hawana budi kujenga ndani mwao ari na moyo wa amani
na kuachana kabisa na falsafa ya vita inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu
wasiokuwa na hatia.
Hii ni sehemu ya mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko
wakati wa Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu
Martha kilichoko mjini Vatican, siku ya Jumanne, tarehe 25 Februari 2014. Baba Mtakatifu
anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwongokea Mwenyezi Mungu na kusali
kwa ajili ya kuombea amani.
Watu watambue udhaifu wao, ili waweze kukimbilia
huruma na upendo wa Mungu; wasikitishwe na maafa ya watu wasiokuwa na hatia. Watu
wasifanye mazoea na vita!