Maaskofu wanashirikishana mang'amuzi kuhusu umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa
wafuasi wa Kristo!
Maaskofu Marafiki wa Chama cha Kitume cha Wafokolari kutoka Afrika, Asia, Mashariki
ya Kati, Amerika na Ulaya wako mjini Castel Gandolfo wakiendelea kushirikishana: uzoefu
na mang'amuzi ya umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa wafuasi wa Yesu Kristo.
Baadhi ya Maaskofu wanaotoka katika nchi ambazo bado kuna vita na kinzani za kijamii.
Maaskofu wanashirikishana juu ya mchango wa Kanisa katika kukuza na kudumisha majadiliano
ya kidini na kiekumene mintarafu changamoto za Uinjilishaji Mpya.
Baadhi ya
viongozi wametoa mada inayogusia ufahamu wa Kanisa mintarafu mwono na maelekeo ya
Baba Mtakatifu Francisko, mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki.
Maaskofu wanaangalia pia umuhimu wa Sinodi za Maaskofu kadiri ya Mafundisho ya Papa
Francisko.
Mkutano huu wa Maaskofu umefunguliwa rasmi hapo tarehe 24 Februari
na utahitimishwa hapo tarehe 28 Februari 2014 baada ya kukutana na kuzungumza na Baba
Mtakatifu Francisko, hapo tarehe 27 Februari 2014.