Kardinali George Pell ateuliwa kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa linaloratibu
masuala ya uchumi na fedha
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali George Pell, Askofu mkuu wa Jimbo kuu
la Sydney, Australia kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa linaloratibu Uchumi na Fedha
ya Vatican baada ya kupata ushauri kutoka kwa Makardinali katika mkutano wao uliohitimishwa
hivi karibuni mjini Vatican.
Kardinali Pell alizaliwa kunako tarehe 8 Juni
1941. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, alipadrishwa kunako tarehe 16
Desemba 1966. Tarehe 21 Mei 1987 akawekwa wakfu kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu
la Melbourne, Australia. Tarehe 16 Julai 1996 Papa Yohane Paulo wa Pili akamteuwa
kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Melbourne. Tarehe 26 Machi 2001 akateuliwa kuwa ni
Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Sydney. Tarehe 28 Septemba 2003 akasimikwa kuwa ni Kardinali.
Kardinali Pell ni kiongozi mwenye uzoefu mkubwa katika masuala ya uchumi na
fedha. Amekuwa ni kati ya Makardinali washauri wa Papa Francisko katika mchakato wa
marekebisho ya kina mjini Vatican. Amekuwa ni kiongozi aliyejipambanua katika mikakati
ya maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili; mshauri katika masuala ya maadili ya
biashara, haki jamii pamoja na maisha ya hadhara.